UDART NA DART MALIZENI CHANGAMOTO YA USAFIRI JIJINI DAR ES SALAAM - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, October 12, 2025

UDART NA DART MALIZENI CHANGAMOTO YA USAFIRI JIJINI DAR ES SALAAM


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amekutana na viongozi wapya wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) na kuwataka kutatua changamoto ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam kwani Serikali imewezesha upatikanaji wa mabasi mapya.

Waziri Mchengerwa amesema, moja ya changamoto iliyokuwa ikikwamisha huduma ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam ni matumizi ya lugha mbaya ya watumishi waliopewa dhamana kuwahudumia wananchi kupitia mabasi ya mwendokasi.

“Wananchi wengine wanakasilika tu kwasababu ya lugha mbaya ya watendaji wetu wa mabasi ya mwendokasi, mtu amekaa masaa kadhaa kwenye kituo alafu matumizi ya lugha yanakuwa si mazuri kwanini asikasirike.”

Ili kuondokana na changamoto hiyo Mhe. Mchengerwa amewataka viongozi hao wapya kutoka ofisini na kwenda kufanya ufuatiliaji utakaobaini mienendo ya watumishi inayopelekea kuibua kero na changamoto zinazokwamisha huduma ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Waziri Mchengerwa amewataka viongozi hao wa DART na UDART kushirikiana kiutendaji, na iwapo wanaona kuna changamoto zinazowakabili kiutendaji wasisite kuwasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI ili kuona namna bora ya kuzitatua changamoto hizo.

Waziri Mchengerwa ameongeza kuwa, mara baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko ya uongozi wa DART na UDART wananchi wamejenga imani kuwa huduma ya usafiri itazidi kuboreka jijini Dar es Salaam, hivyo ametoa rai kwa viongozi hao kuhakikisha wanailinda na kuiishi imani hiyo kwa vitendo.

Sanjari na hilo, Waziri Mchengerwa amewataka viongozi hao kuhakikisha wanatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa Oktoba 02, 2025 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka kwa njia ya Kivukoni hadi Kimara.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka viongozi hao kuhakikisha majaribio ya njia ya mbagala yanakamilika kwa wakati na wakamilishe mchakato wa kusaini mikataba ya wawekezaji, ili wakazi wa mbagala nao wapate huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) Balozi Dkt. Ramadhani Kitwana Dau amemhakikishia Mhe. Mchengerwa kuwa viongozi wa UDART na DART watatekeleza maelekezo aliyoyatoa kwa kufanya kazi kwa ushirikiano ili kutatua changamoto ya usafiri jijini Dar es Salaam.

"Ninaamini ndani ya miezi sita changamoto zote zilizokuwepo zitabaki kuwa historia, ni kweli changamoto zipo lakini zinatatulika ndani ya miezi mitatu na kwa kiasi fulani tumeanza kupata pongezi ya maboresho ya huduma mara baada ya kuchukua hatua," amesisitiza Balozi Dau.

Katika kikao kazi hicho cha kuhimiza uwajibikaji, Waziri Mchengerwa amefanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya DART Bw. David Kafulila na mwenyekiti wa Bodi ya UDART Balozi, Dkt. Ramadhan Dau, Pamoja na Watendaji Wakuu wa taasisi hizo.


No comments:

Post a Comment