Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata watuhumiwa wanne katika eneo la Mlalakuwa, Kinondoni wakiwa wanatengeneza biskuti za bangi kwa ajili ya house party ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
Watuhumiwa hao ni Bright A. Malisa, Humphrey G. Safari, Novatus A. Kileo, na Chriss P. Mandoza, wote wakiwa na umri wa miaka 26.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 21, 2025 Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema watuhumiwa walikutwa na biskuti 140 za bangi, puli nane, na paketi tisa za bangi zenye jumla ya kilo 2.858.
"Hii inaonesha namna vijana wetu wanavyohatarisha maisha yao kwa kujihusisha na utengenezaji wa bidhaa zenye dawa za kulevya kwa ajili ya starehe,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Aidha, amesema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaendelea na uchunguzi wa matumizi ya bangi kwenye bidhaa mbalimbali ikiwemo vinywaji, vyakula, vipodozi na sigara za kielektroniki (vapes), ambapo baadhi ya bidhaa zimebainika kuwa na viambata vya bangi.
Pamoja na hayo amesema Mamlaka imekamata jumla ya kilogramu 10,763.94 za aina mbalimbali za dawa za kulevya pamoja na kilogramu 6,007 na lita 153 za kemikali bashirifu, huku watuhumiwa 89 wakikamatwa kuhusiana na uhalifu huo.
Amesema katika operesheni iliyofanyika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, Mamlaka ilikamata dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilogramu 40.32 zilizokuwa zimekaushwa na kufungwa kama viungo (spices) katika paketi 80 zenye maandishi ya “Dry Basil Leaves”. Dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa kwenda nchini Canada na Italy kupitia makampuni ya usafirishaji.
Ametaja waliokamatwa kuhusiana na dawa hizo kuwa ni Yusuphu S. Kibaha (35) na Mohamed H. Ramadhan (41), na uchunguzi wa awali umebaini dawa hizo ziliingizwa nchini kwa njia za kificho kutoka nchi jirani.
“Uchunguzi wetu umeonesha uwepo wa mtandao wa usafirishaji wa mirungi unaotumia bodaboda na baadhi ya mawakala wa kampuni za usafirishaji ili kurahisisha kusafirisha dawa hizo bila kutiliwa shaka. Mtandao huu unaweza kuathiri taswira ya nchi yetu kimataifa, na sisi hatutalifumbia macho suala hili” ameonya Kamishna Jenerali Lyimo.
Akizungumzia operesheni zilizofanyika mikoani, Lyimo amesema DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imefanikiwa kukamata bangi kilo 9,164.92, mirungi kilo 1,555.46, skanka gramu 367, na heroin gramu 7.498, pamoja na kuteketeza ekari 11.5 za mashamba ya bangi.
Aidha, amewaonya bodaboda, wamiliki wa kampuni na mawakala wa usafirishaji kuwa makini na mizigo wanayobeba au kusafirisha ili kuepuka kujikuta kwenye mgogoro wa kisheria. Pia ametumia fursa hiyo kuwaonya wanafunzi wa vyuo vikuu kuacha mara moja kujihusisha na dawa za kulevya na badala yake kutumia muda wao katika masomo ili kutimiza ndoto zao.
“Vijana wetu ndio nguvu kazi ya taifa. Tunataka waishi maisha yenye afya, wasikubali kudanganywa na makundi yanayotumia dawa za kulevya kama sehemu ya starehe. Mamlaka haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayehusishwa na uhalifu huu,” amesema












No comments:
Post a Comment