WAAJIRI WATAKIWA KUZINGATIA MAFUNZO YA MAADILI KWA WATUMISHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 2, 2025

WAAJIRI WATAKIWA KUZINGATIA MAFUNZO YA MAADILI KWA WATUMISHI


Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais–Utumishi, Bi. Hilda Kabissa,
akifungua kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa maadili na utawala bora kati ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka za kitaaluma , Oktoba 2, 2025 jijini Dodoma


NA OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali imewataka watumishi wa umma nchini kuzingatia sheria, kanuni, taratibu pamoja na maadili ya kitaaluma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, zenye weledi na heshima.

Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais–Utumishi, Bi. Hilda Kabissa, ambaye alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, wakati akifungua kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa maadili na utawala bora kati ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka za kitaaluma.

Bi. Kabissa amesema Ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya watumishi wa umma kutoa huduma zisizoridhisha ikiwemo kutumia lugha zisizofaa, kudharau utu wa wateja na kutoa majibu yanayokatisha tamaa.

“Tabia hizi ni kinyume na misingi ya sheria na maadili ya utumishi wa umma. Ni lazima tubadili mtazamo ili kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao,” amesisitiza.

Aidha, amewakumbusha waajiri wote nchini kuhakikisha mafunzo ya maadili yanapewa kipaumbele kwa watumishi wapya na waliopo kazini, akibainisha kuwa baadhi ya ofisi za umma zimeshindwa kutenga au kutumia ipasavyo fedha za mafunzo yaliyopangwa kwenye bajeti kupitia Lengo B (kukuza uadilifu na juhudi dhidi ya rushwa).

“Ukosefu wa kipaumbele katika mafunzo haya umechangia kuwepo kwa watumishi wasiokuwa waadilifu na wasiokuwa na weledi wa taaluma, hali inayorudisha nyuma juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa,” amesema.

Vilevile, Bi. Kabissa amesisitiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utoaji huduma za Serikali, akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika matumizi ya teknolojia ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na kupunguza mianya ya rushwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais–Utumishi, Bi. Felister Shuli, amesema kikao hicho ni utekelezaji wa maazimio ya vikao vya awali vya kubadilishana uzoefu kati ya taasisi husika.

“Kama ilivyoazimiwa mwaka 2023, vikao hivi hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa utaratibu wa kubadilishana. Mwaka huu TAKUKURU wameratibu kikao cha tano, na sasa OR-UTUMISHI ndiyo mwenyeji wa kikao hiki cha sita,” amesema.

Bi. Shuli ameongeza kuwa vikao hivyo ni jukwaa muhimu la kujadili changamoto na kubadilishana mbinu za kusimamia maadili ya utendaji na kitaaluma kwa watumishi wa umma.

Kikao kijacho kinatarajiwa kuratibiwa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT) mwezi Machi 2026.






No comments:

Post a Comment