
Na Sixmund Begashe, Dar es Salaam
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amezindua onesho maalum la Historia ya Reli ya Tanzania–Zambia (TAZARA) katika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, jijini Dar es Salaam linalolenga kuelimisha vizazi vya sasa na vijavyo kuhusu uongozi wa maono wa waasisi wa Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa onesho hilo litakalofanyika kwa miezi miwili, Dkt. Kijaji amesema onesho hilo ni darasa hai kwa vizazi hivyo ili kujifunza mchango wake katika maendeleo na ukombozi wa kiuchumi wa ukanda huo.
Amebainisha kuwa TAZARA, iliyojengwa mwaka 1970 kwa ushirikiano na Serikali ya China, ni alama muhimu ya mshikamano kati ya Afrika na China, na kwamba imeendelea kuwa miongoni mwa miundombinu yenye mafanikio makubwa katika kusafirisha watu na bidhaa kati ya Tanzania, Zambia na China.
"Haya ni matunda ya waasisi wetu ambao wameturithisha. Sasa tunayahifadhi na kuyaendeleza vyema chini ya Mhifadhi wa Urithi wetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, Waziri huyo amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutembeleaonesho hilo, akisema kufanya hivyo ni sehemu ya kuenzi urithi wa taifa, kudumisha amani, utu na mshikamano wa kitaifa kwa manufaa mapana ya Watanzania.
Uzinduzi huo pia, umehudhuriwa na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian, mabalozi mbalimbali, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga, pamoja na viongozi na wananchi ambapo onesho hilo linajumuisha michoro, machapisho na mikusanyo mbalimbali ya kihistoria huku likipambwa na burudani ya ngoma za asili.







No comments:
Post a Comment