
NA Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amesema Wizara hiyo inahitaji watumishi wenye kuleta matokeo, wanaoamini kuwa inawezekana na wasiotoa visingizio katika utekelezaji wa majukumu yao, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji.
Waziri Aweso ametoa kauli hiyo leo, Februari 27, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na Vyombo vya Utoaji wa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs).

Mkutano huo uliambatana na uzinduzi wa miongozo ya utoaji huduma ya maji vijijini pamoja na taarifa ya utendaji kazi ya CBWSOs ya mwaka 2024/2025.
Miongoni mwa miongozo iliyozinduliwa ni Mwongozo wa Fedha, Mwongozo wa Utumishi na Mwongozo wa Ununuzi, yote ikiwa na lengo la kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma ya maji vijijini.
Katika hatua nyingine, Aweso amewaalika wadau wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali kufikisha huduma ya maji katika vijiji 1,575 ambavyo bado havijafikiwa, ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Amesema umefika wakati kwa sekta binafsi kuweka nguvu zaidi katika sekta ya maji kama ilivyo katika sekta nyingine, ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha huduma ya maji inapatikana katika vijiji vyote ifikapo mwaka 2030.
“Umefika wakati sasa wa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma ya maji, na sisi Serikali tutahakikisha tunasimamia usalama na gharama za maji. Lengo ni kuhakikisha vijiji vyote 1,575 ambavyo havijafikiwa vinapata huduma hiyo,” amesema Aweso.
Ameongeza kuwa Serikali inataka ifikapo mwaka 2030, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan atakapomaliza muda wake wa uongozi, maeneo yote yawe yanapata huduma ya maji bila vikwazo.
Katika hatua nyingine, Aweso ameisisitiza RUWASA kusimamia kwa karibu miradi zaidi ya 3,000 inayoendelea kutekelezwa katika vijiji mbalimbali nchini, akibainisha kuwa Serikali imetoa fedha nyingi kugharamia miradi hiyo.
Amesema miradi hiyo itakapokamilika itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini.
“Hadi sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini imefikia asilimia 85.2, na Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kuhakikisha maeneo yote yanafikiwa na kupata huduma hiyo pasipo vikwazo,” amesema.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kufunga mita za maji za kulipia kabla ya matumizi (prepaid meters) kwa lengo la kudhibiti upotevu wa maji na kuongeza mapato ya makusanyo.
Ameeleza kuwa Rais Dk. Samia amefanya kazi kubwa ya kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kufanya kazi kwa uzalendo ili miradi hiyo ilete tija iliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amezitaka CBWSOs kushughulikia kero zote zinazosababisha wananchi kukosa huduma ya maji bila sababu za msingi.“Nawaomba mkashughulikie changamoto zilizopo katika maeneo yenu. Kuna maeneo maji yanavuja kwa wiki nzima bila kushughulikiwa, na yapo maeneo wananchi wanakosa maji kwa miezi miwili kwa sababu pampu imeharibika au umeme wa Luku umekatika. Nendeni mkamalize changamoto hizo ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama,” amesema.
Amesisitiza wataalamu katika vyombo hivyo kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia taaluma zao ili kufikia malengo ya Serikali ya kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa wote.

Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Wolta Kirita, amesema mafanikio yamepatikana ambapo upatikanaji wa maji safi na salama vijijini umeongezeka kutoka asilimia 64.8 mwaka 2019 hadi asilimia 85.2 Desemba 2025.

Naye Mwenyekiti wa CBWSOs, Nicholaus Kombe, amesema mkutano huo umewawezesha kufahamu matarajio ya wizara na kujifunza mbinu bora za kuboresha utoaji wa huduma ya maji ili kuhakikisha jamii inapata maji safi na salama kwa wakati.









No comments:
Post a Comment