
Jumla ya Sh12.4 bilioni zimetolewa na NMB Bank Plc kwa wafanyabiashara zaidi ya 6,011, huku wanufaika wakipatiwa pia elimu ya fedha na uongozi ili kuwaongezea uwezo wa kusimamia mikopo na kukuza biashara zao.
Takwimu hizo zimetolewa na Meneja Mwandamizi wa Idara ya Biashara za Serikali wa NMB, Amanda Feruzi, katika mkutano wa Jumuiya ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa Ukanda wa Ziwa Victoria (LVRLAC) unaoendelea katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma.
Fedha hizo ni sehemu ya Sh13 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa NMB kwa ajili ya utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, katika mfumo wa majaribio unaotekelezwa katika halmashauri sita.
Halmashauri zilizochaguliwa katika awamu ya majaribio ni Majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, Manispaa ya Songea, pamoja na Halmashauri za Newala, Bumbuli na Itilima.
Feruzi amesema NMB iko tayari kuendelea kushirikiana na jumuiya hiyo, kama ilivyofanya kwa miaka iliyopita kupitia udhamini na ushiriki katika mikutano yao ya kila mwaka.
Ameongeza kuwa benki hiyo imekuwa mshirika wa Serikali katika utekelezaji wa miradi ya uwezeshaji wa makundi maalum kupitia fedha zinazotengwa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Alisema NMB ina uzoefu katika masuala ya hati fungani (APF), ikiwa ni benki ya kwanza nchini Tanzania na Afrika Mashariki kutoa hati fungani ya Jinsia (Jasiri Bond) na ya Uendelevu (Jamii Bond), ambazo zimevutia wawekezaji wa ndani na nje katika masoko ya mitaji ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, NMB pia ilikuwa benki ya kwanza kuunganishwa katika mfumo wa malipo wa Serikali (GePG), hatua iliyorahisisha ukusanyaji wa mapato kupitia uwekezaji mkubwa katika teknolojia, bidhaa na huduma mbalimbali, na kuifanya kuwa mstari wa mbele katika ubunifu wa suluhisho za kifedha kwa wateja na Serikali.
Akizungumza katika mkutano huo uliowakutanisha wajumbe 42 kutoka mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera, Feruzi aliwataka viongozi wa serikali za mitaa kutumia fursa ya kutafuta mitaji kutoka kwa wawekezaji ili kuanzisha vyanzo vipya vya mapato.
Alisema benki inaishauri Serikali kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati kwa kushirikiana na sekta binafsi kupitia ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP) pamoja na hati fungani za miradi (APF).
Baadhi ya manufaa ya mfumo huo ni pamoja na kuharakisha maboresho ya miundombinu, kupunguza utegemezi wa bajeti kuu ya Serikali, kuruhusu utekelezaji wa miradi kwa wakati, na kunufaika na uzoefu wa sekta binafsi katika upatikanaji wa mitaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Reuben Kwagilwa, aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kufanya kazi kwa ushirikiano na sekta binafsi, huku akisisitiza umuhimu wa kuitumia NMB katika kupata suluhisho za kifedha.
Aidha, alionya kuwa Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayebainika kulegalega katika matumizi ya fedha za umma, na kuwataka wakurugenzi kulipa madeni ya jumuiya kwa wakati pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi bila kusubiri viongozi wa juu kufika katika maeneo yao.




No comments:
Post a Comment