
Zaidi ya kaya 700 zimeathiriwa na mafuriko katika Kata ya Mhonda Tarafa ya Turiani, Wilaya ya Mvomero, kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Akizungumza katika eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Maulid Doto amewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema, ikiwemo kuhama katika maeneo yaliyo karibu na mto unaotajwa kuwa chanzo cha mafuriko hayo, ili kuepusha madhara zaidi.
Aidha, amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuweka kambi maalum ya tathmini na utafiti wa kina, kubainisha mipaka ya maeneo yaliyoathirika pamoja na kuyatambua rasmi maeneo hatarishi kwa lengo la kupanga hatua madhubuti za kudhibiti madhara ya mafuriko siku zijazo.
Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Sara Msafiri Ally, akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Maulid Doto, pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri na viongozi wengine wa serikali, wamefika katika eneo la Kichangani, Tarafa ya Turiani, kujionea athari za mafuriko hayo na kuwapa pole wananchi waliokumbwa na janga hilo.
Katika hatua ya kuwafariji na kuwasaidia waathirika, Mbunge huyo amechangia kiasi cha shilingi milioni tano ili kusaidia mahitaji ya haraka kwa familia zilizoathirika, wakati serikali ikiendelea kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu ikiwemo mpango wa kuwahamisha wananchi kutoka maeneo hatarishi na kuwapeleka katika maeneo salama zaidi.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, George Pindua, amesema kuwa katika nyakati za majanga kama haya, jamii haina budi kuwa na mshikamano na kusaidiana bila kujali tofauti za dini au itikadi, akisisitiza kuwa maafa hayachagui mtu wala dini.
Serikali na wadau mbalimbali wanaendelea kushirikiana kuhakikisha waathirika wanapata msaada wa haraka huku hatua za kudumu zikichukuliwa kuzuia madhara kama hayo kujirudia.






No comments:
Post a Comment