
Na Shua Ndereka, Morogoro
Ushiriki wa wananchi mkoani Morogoro na nje ya mkoa, katika maonesho ya Biashara mkoani hapa unatarajia kuchangia na kukuza biashara za ndani, kuimarisha ubunifu na kuleta maendeleo chanya kwa uchumi wa Mkoa wa Morogoro.
Maonesho hayo katika Mkoa wa Morogoro yameandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Morogoro, kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, yanatarajiwa kuanza Novemba 20 hadi Novemba 30 mwaka huu, katika uwanja wa Jamhuri Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema, Mkoa wa Morogoro ni kitovu cha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ikiwemo zao la Chikichi ambalo lilibuniwa na kusambazwa kwa miche zaidi ya milioni moja Morogoro vijijini, licha ya zao hilo kupitwa sasa na mazao mengine kama; Karafuu na Kakao ambapo baada ya mkoa wa Mbeya kwa uzalishaji wa kakao mkoa wa Morogoro unashika nafasi ya pili huku Zanzibar ikiongoza kwa Karafuu na kufuatiwa na mkoa huu.
“ushiriki wa wananchi katika maonesho hayo utachangia ukuzaji wa Uchumi, kupitia kuimarisha bunifu kwa wajasiriamali na kuleta maendeleo kwa jamii, kukuza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo na uzalishaji viwandani ili kuongeza tija endelevu na ushindani wa kikanda”.
Aidha Maonesho hayo ni jukwaa la kuwakutanisha wafanyabiashara, taasisi za serikali na binafsi, wawekezaji wadau wa maendeleo kwa ajili ya biashara na kujenga mitandao na kukuza ushirikiano.

Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Morogoro Muadhini Mnyanza amesema, Zaidi ya washiriki 198 wamethibitisha kushiriki maonesho hayo, ikiwa wajasiriamali 156, taasisi za umma zaidi ya 17 na wafanyabiashara wa kati 32 wanatarajia kushiki katika maonesho ya Biashara ya mkoa wa Morogoro ‘The Morogoro Region Trade Fair Exhibition (MRTFE) 2025.
Pia maonesho hayo yanakusudia kutoa elimu ya uchumi na biashara kupitia Semina, warsha na midahalo ya kitaalamu ya sekta mbalimbali na jukwaa la kuonesha bidhaa, huduma za ubunifu katika sekta za biashara, viwanda na kilimo.
TCCIA Morogoro imewataka wadhamini na waoneshaji kujitokeza mapema kwa kuwa nafasi za mabanda ni chache, ikiwa maandalizi ya awali yanaendelea vizuri huku huduma za ziada ikiwemo afya na vitambulisho vya taifa (NIDA) zitatolewa bure katika maonesho hayo.
Imefafanua kuwa maandalizi ya awali yamehusisha taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya serikali pamoja na makampuni binafsi kwa lengo la kutoa huduma bora wakati wa maonesho.
Hata hivyo Maonesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Novemba 24, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima huku yakibebwa na kauli mbiu isemayo“Kukuza ujasiriamali, ubunifu na uwekezaji wa kimkakati kwa maendeleo Jumuishi ya Uchumi” ikiwa na lengo la kuimarisha mchango wa sekta binafsi na kuhamasisha uwekezaji ndani ya mkoa.

No comments:
Post a Comment