NMB Yawatambua wanafunzi Ubora na Kuimarisha Ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 18, 2025

NMB Yawatambua wanafunzi Ubora na Kuimarisha Ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam


Benki ya NMB kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Biashara, imewatambua wanafunzi kumi bora katika kozi kumi waliomaliza masomo mwaka huu kwa hafla maalum ya utoaji wa zawadi mbalimbali, ikiwatambua kwa mafanikio yao ya kitaaluma na juhudi kubwa iliyowaletea ufaulu.

Hafla iliyofanyika siku moja kabla ya kuanza kwa mahafali za chuo hicho, zawadi za pesa taslimu, vyeti na fursa za mafunzo kazini kwa washindi hao zilitolewa na Benki ya NMB huku wawakilishi wa Benki hiyo wakipongeza juhudi kubwa za wahitimu na chuo kwa ujumla katika dhamira yao ya kukuza vipaji na maendeleo ya kitaalamu.

Kwa niaba ya Benki ya NMB, Mgeni Rasmi wa shuguli hiyo, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Kituo cha Utaalamu wa Benki ya NMB, Joanitha Mrengo, alielezea fahari ya Benki katika kuunga mkono juhudi mbalimbali za vijana na hususani za kitaaluma ambazo zitazaa watalaamu bora kwa maslahi ya taifa kwa ujumla.

“Kwetu sisi ni fahari kubwa kushiriki katika kutambua bidii na juhudi za vijana hawa wadogo, alisema joanitha.

“Leo hii tunashuhudia nidhamu, uvumilivu na ubora wao wa kitaaluma ukileta majibu stahiki. Benki ya NMB itatengeneza fursa kuanzia za ajira na hata za mafunzo kazini ambazo tunaamini zitawawezesha wataalamu hawa kustawi katika soko la ajira.”

Mrengo aliongeza kuwa Benki ya NMB inaendelea kujivunia ushirikiano wa dhati uliopo baina ya taasisi hiyo ya fedha na chuo kikuu cha dar es salaam kwani wameshafanya mengi ikiwemo kutoa fursa za kuwapa wanafunzi nafasi za kujifunza wakiwa masomoni katika benki hiyo na hivyo kuchangia katika kuzalisha wataalamu zaidi katika sekta ya kifedha.

“Mbali na mafunzo wakiwa kazini watakayopata washindi wetu wa leo, tumekuwa na ushirikiano na Chuo kikuu cha Dar es Salaam katika kuendelea kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa chuo hiki. Lakini pia tunayo makubaliano makubwa ya kuendelea kushirikiana katika masuala ya kitehama,” Alisema Mrengo.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Utafiti, Profesa Nelson Boniface, pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo akisema, “Ushirikiano wetu na Benki ya NMB unaboresha ubora wa elimu tunayoitoa na unachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taifa. Pamoja, tunatengeneza viongozi watakaochochea maendeleo ya Tanzania.”

Naibu Makamu Mkuu pia alibainisha kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitatumia wataalamu mbalimbali ikiwemo wale wa NMB kutoa mihadhara maalum, ili kuwapa wanafunzi maarifa ya vitendo katika nyanja zao.

Jitihada hizi zikilenga kuwapa wanafunzi elimu ya kitaaluma pamoja na maarifa halisi ya kazi, kuwapa wanafunzi mtazamo mpana zaidi nje ya darasa na kuwaandaa vyema kwa changamoto zijazo.

Mkuu wa Idara ya Wanafunzi wa Chuo, Profesa Omary Mbura, alielezea nafasi ya NMB kama mshirika wa kina: “Benki ya NMB imekuwa ikituunga mkono si tu kwa msaada wa kifedha bali pia kwa kushiriki kikamilifu katika miradi yetu ya kitaaluma na jamii,” alisema.

Ushirikiano kati ya Benki ya NMB na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unaakisi dhamira ya pamoja ya ubora, ubunifu na ukuaji kwa Taifa.

Wakati chuo kinaendelea kulea viongozi wa kesho, ushirikiano huu ni hatua ya kimkakati kuelekea kuleta mafanikio makubwa ya kitaaluma na yenye tija kwa taifa kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja wa Benki ya NMB kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio alisema, “Tunatarajia kuimarisha zaidi uhusiano huu, ambao unawanufaisha si tu wanafunzi na wafanyakazi wa chuo bali pia unachangia katika maendeleo ya uchumi wetu na kwa pamoja, tunajenga mustakabali mzuri wa Tanzania.”

No comments:

Post a Comment