
Na Mwandishi Wetu, Mahenge, Morogoro
Imeelezwa kwamba uwepo wa miradi ya graphite Mahenge, Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro itafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kuanzia ngazi ya kijiji mpaka taifa kutokana na uwekezaji mkubwa unaotarajiwa kuwekezwa katika maeneo yaliyothibitishwa na kampuni mbili za uwekezaji Faru Graphite na Duma Graphite kupitia kampuni ya TanzGraphite.
Hayo yalibainishwa Novemba 11, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Juma Kapilima wakati akielezea kuhusu fursa za kiuchumi na kijamii zitakazojitokeza kupitia uwekezaji mkubwa unaotarajia kufanyika katika miradi ya madini ya kinywe.
Kapilima alisema kuwa, mradi wa faru graphite unatarajia kuleta ajira 900 za moja kwa moja na ajira 4000 zisizo za moja kwa moja ambapo kupitia nafasi hizo kutafungua ajira nyingine ndogo ndogo kwa jamii ya Mahenge na viunga vyake.
Akielezea kuhusu ujenzi wa miundombinu ya nishati ya umeme, Kapilima alisema kuwa, kupitia mradi huo kuna mpango wa kuvuta umeme wa kilovoti 220 kutoka Ifakara hadi Mahenge ikiwa pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara zitakazo unganisha eneo la mradi na vitongoji na vijiji ili kurahisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Faru Graphite Jacqueline Mushi alisema kuwa, utekelezaji wa Mpango wa Wajibu wa Kampuni (CSR) tayari umeanza mpaka sasa umejenga Ofisi za vijiji 3 ikiwa ni kijiji cha mdindo, kisewe na mdindo.
Pia mradi umechangia mifuko 100 ya simenti kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Makanga pamoja na ukarabati wa shule ya msingi Makanga na uchimbaji wa visima katika kijiji cha mdindo.
Mushi aliongeza kuwa, Mradi wa Faru unalenga kusimama katika mwelekeo wa kombe la uchumi wa kijani hii ni kutokana umuhimu wa malighafi ya graphite hususan katika matumizi ya vifaa vya teknolojia ambayo kupitia mradi Tanzania ina nafasi ya kuingia katika mnyororo wa thaman ya kimataifa wa teknolojia safi.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mdindo, Nestory Uhadi alieleza kuwa eneo la Mahenge lina miradi miwili mikubwa ila kwa upande wa mradi wa Faru , umekuwa na matumaini makubwa kwa jamii, mpaka sasa tayari waguswa zaidi ya 1200 waliopisha mradi wamelipwa fidia, madarasa saba ya shule ya msingi Makanga yamefanyiwa ukarabati na Ofisi Mbili za kijiji zimejengwa kupitia mradi wa Faru Graphite.
Nestory aliongeza kuwa, kupitia ushirikiano mzuri uliopo baina serikali ya kijiji na kampuni za uwekezaji inaleta matumaini makubwa ya maendeleo ndani ya maeneo yetu na wananchi kwa ujumla.






No comments:
Post a Comment