MSIMU WA SABA WA MASHINDANO YA RIADHA YA WANAWAKE KUANZA RASMI NOVEMBA 28 MKAPA STADIUM DAR ES SALAAM - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 26, 2025

MSIMU WA SABA WA MASHINDANO YA RIADHA YA WANAWAKE KUANZA RASMI NOVEMBA 28 MKAPA STADIUM DAR ES SALAAM



Msimu wa saba wa mashindano ya Riadha ya Wanawake utafanyika Novemba 28 hadi 30, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mashindano hayo yatafanyika kwa siku mbili Novemba 29 na 30 na yatatanguliwa na semina kwa wanariadha na waamuzi itakayofanyika Novemba 28 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza Leo Novemba 26, 2025 na waandishi wa habari, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Bi. Neema Msitha, amesema maandalizi yote yamekamilika ambapo amebainisha kuwa mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi,Pia kutakuwepo na viongozi kutoka Japan, JICA, Shirikisho la Riadha Tanzania (AT) na taasisi nyingine.


“Tunafahamu kuwa ushiriki wa wanawake katika michezo bado uko chini ukilinganisha na wanaume, licha ya juhudi za Serikali na wadau mbalimbali kupambana na hali hiyo,” amesema Neema.






Ameongeza kuwa mashindano hayo yatashirikisha wanariadha 155 kutoka mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar, watakaoshindana katika mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1500, 5000, mbio za kupokezana vijiti (4×100m) pamoja na kurusha mkuki.

Aidha, mashindano hayo yataambatana na matukio mbalimbali ikiwemo mafunzo ya matumizi ya taulo za kike, nidhamu ya matumizi ya fedha pamoja na upimaji wa afya kwa washiriki.

“BMT linamshukuru sana Kanali mstaafu na mwanariadha wa zamani, Jumaa Ikangaa, kwa kuyaanzisha mashindano haya kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia JICA. Mashindano haya yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya wanariadha wa kike ambao wengi wameiwakilisha nchi kimataifa,” amesema Neema.

Ametoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji na kutoa hamasa kwa wanariadha wa kike wanaokuza mchezo wa riadha nchini.

No comments:

Post a Comment