
Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati Mhe. Salome Makamba ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuimarisha njia bora na ya haraka ya usafirishaji wa Mafuta nchini ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa mafuta.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Makamba alipofanya kikao kazi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Jijini Dodoma.
Mhe. Makamba amesisitiza uwepo wa maghala ya kutosha ya kuhifadhia mafuta Nchini ili Wananchi waepukane na changamoto ya ukosefu wa Mafuta na kupongeza jitihada za kukabiliana na changamoto hii ambayo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuidhibiti.
Sambamba na hilo Mhe. Makamba ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuangalia namna bora ya upunguzaji gharama za Vifaa vya uwekaji wa mifumo ya umeme majumbani ili kuongeza Idadi ya watumiaji wa Nishati hiyo hasa maeneo ya vijijini.
Vilevile Mhe. Makamba amesisitiza Mamlaka hiyo kuangalia namna bora ya kutoa fursa mbalimbali hasa kwa kundi la Vijana ili kupunguza wimbi kubwa la Vijana wasiokuwa na ajira nchini Tanzania na kuwashirikisha fursa mbalimbali zilizoko kwenye sekta ya nishati nakuwajengea uwezo kwenye miradi.
Nae Dkt. James Andilile Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ameeleza kazi mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo ikiwa ni pamoja na Kudhibiti Ubora, Usalama na tija ya watoa huduma vilevile kutathimini na kurekebisha bei za huduma. Sambamba na vipaumbelee watavyovisimamia ndani ya siku ya miamoja ikiwa ni kutekeleza agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hasaan.
“Sisi kama Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji tutaendelea kuweka mizania ya maslahi sawa kati ya Wadau husika na hivyo kuchochea ongezeko la tija, ushindani, na upatikanaji wa huduma bora kwa wote lakini pia tutaendelea kuzingatia misingi mikuu ya Utawala bora katika maamuzi ya Udhibiti ambayo ni weledi, uwajibikaji, Utabirikaji, Ushirikishwaji wa wazi na kufuata Sheria.” Amesema Dkt. Andilile




No comments:
Post a Comment