
Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Morogoro umeanza matengenezo ya mfumo wa kupima uzito wa magari yakiwa kwenye mwendo (WIM) katika mizani ya Mikese ili kuondoa msongamano wa magari katika Barabara Kuu ya Morogoro.
Ufungaji wa Mizani hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali yaliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, wakati akiwa katika ziara ya kikazI ya ukaguzi wa miradi na kushuhudia msongamano mkubwa wa magari na kuelekeza timu ya watalaamu kufika mara moja na kuanza kushughulikia tatizo hilo.
Akizungumza leo Novemba 24, 2025 Mtaalam wa Mizani kutoka TANROADS, Mhandisi Juma Kipande, ameeleza kuwa changamoto kubwa ya mzani huo ni kuharibika kwa sensor ya mizani hali iliyopelekea mzani kushindwa kupata uzito sahihi wa uzito wa magari.
"Mzani huu ulifungwa kama moja majaribio ya Wizara mwaka 2015 lengo likiwa ni kupunguza msongamano katika vituo vya mizani na hivi sasa tumeufungua na kuanza kuurekebisha ili huduma ziendelee haraka", amefafanua Mhandisi Kipande.
Novemba 23, 2025 Waziri Ulega alifanya ziara ya kushtukiza katika mzani huo na kubaini hitilafu katika mfumo wa WIM na kuwataka TANROADS kurekebisha kasoro hizo haraka iwezekanavyo pamoja na kuwasimamisha watumishi wazembe kwa lengo la kupisha uchunguzi na hatua za kinidhamu zitachukuliwa.

No comments:
Post a Comment