
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa siku 10 kwa watendaji wa taasisi zinazohusika na usafiri wa mwendokasi jijini Dar es Salaam wakae na kuainisha maeneo ya kufanyiwa kazi kwa haraka ili kurejesha hali ya mpito wakati Serikali ikitafuta suluhisho la kudumu.
“Wizara ya Ujenzi, TANROADS, DART, UDART, OWM-TAMISEMI, TANESCO na wadau wengine, kaeni kuanzia leo, husisheni mabenki rejesheni intaneti, umeme, mageti ya kukatia tiketi ili turejeshe hali ya mpito wakati tukitafuta suluhisho la kudumu,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo jioni (Jumatatu, Novemba 24, 2025) wakati akizungumza na wakazi wa Dar es Salaam katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mbezi, wilayani Ubungo, jijini humo. Alikuwa katika ziara ya siku moja ya kukagua miundombinu iliyoharibiwa na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025 pamoja na kutoa pole kwa wakazi walioathiriwa na vurugu hizo.
“Nimekuja kutoa pole kwa Watanzania walioathiriwa na tukio hili. Ninaungana na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa wote walioathirika na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025.”
“Tuangalie upya hatua zetu tunazozichukua. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda Tume ili kuliangalia jambo hili, ninawaomba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais na wajumbe wa tume iliyoundwa ili kuchunguza undani tukio la vurugu zilizotokea, tujue namna lilivyofanyika na hatua stahiki zitakazochukuliwa.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Rais ameelekeza kuwa hakutakuwa na maadhimisho ya Sherehe za Uhuru za 09 Desemba na badala yake fedha ambazo zilipaswa kutumika kwenye sherehe hizo zitumike kurekebisha miundombinu iliyoharibika kutokana na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025.
Ameelekeza viongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na sekta zinazohusika wakae na kuratibu fedha hizo ili jambo hilo lifanyike kwa haraka ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais.
Wakati huohuo, Rais Samia ametoa msamaha kwa taasisi za kidini zenye changamoto na kuielekeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilifungulie Kanisa la Ufufuo na Uzima na taasisi nyingine za kidini, na kwamba lipewe miezi sita ya uangalizi katika kuzingatia miiko, masharti na sheria za uendeshwaji wake.
“Waziri wa Mambo ya Ndani, baada ya hapa fuatilia utaratibu mzuri ziandikie upya taasisi za kidini, miiko yao na masharti ya uandikishaji na zile ambazo zilikuwa na shida ziweke kwenye uangalizi wa miezi sita, ipo taasisi ya Ufufuo na Uzima nenda kaifungulie. Ifungulie, wape masharti ya uangalizi ndani ya miezi sita. Ziandikie taasisi zote za kidini kuzikumbusha miiko na mipaka ya ufanyaji kazi, sawa sawa na sheria na Katiba ya nchi yetu,” amesema.
Sambamba na hilo, ameelekeza kurekebishwa kwa sharti linalotaka kufungiwa kwa nyumba ya ibada endapo atakosea kiongozi, akisisitiza kuwa anayekosea ndiye aadhibiwe bila kuathiri waumini kufanya ibada. “Akikosea Sheikh, usiadhibiwe msikiti na akikosea Askofu, wasinyimwe waumini kufanya ibada kwani ibada ni ushirika kati ya mwanadamu na Mungu wake na siyo yeye na askofu au sheikh,” amesema.
Waziri Mkuu aliambatana na Mawaziri na Naibu Mawaziri kutoka Wizara za Mambo ya Ndani, Ujenzi, Mambo ya Nje, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Viwanda na Biashara, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) na Uchukuzi.

No comments:
Post a Comment