
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wakurugenzi wa mipango na sera kutoka wizara zote, wakuu wa idara za uchumi katika ofisi za makatibu tawala wa mikoa, pamoja na wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama, Halmashauri na Manispaa zote nchini, wamepatiwa mafunzo mahsusi kwa ajili ya uandaaji wa mipango mikakati itakayowezesha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Akifungua warsha ya siku mbili kwa wataalam hao, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Dk. Fred Msemwa, alisema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuhakikisha kila taasisi inatengeneza mpango mkakati utakaoendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Dk. Msemwa alisema tathmini ya Dira ya Maendeleo 2025 imeonyesha mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia mipango iliyotekelezwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sekta za elimu, afya, hifadhi ya jamii na huduma nyingine za kijamii.
Hata hivyo, alibainisha kuwa si rahisi mpango wowote kutekelezwa kwa asilimia 100, akifananisha hali hiyo na mipango ya kifamilia ambayo nayo huwa haifiki asilimia zote za utekelezaji.
Ameeleza kuwa kundi lililoshiriki mafunzo hayo linahusisha kada muhimu za wachumi, wanamipango na watakwimu, wataalam wenye jukumu kubwa katika uandaaji wa mipango ya maendeleo ya Serikali.
Akifafanua zaidi, Dk. Msemwa alisema mafunzo hayo yalilenga kuwasilisha muongozo wa kuandaa mipango mikakati katika taasisi mbalimbali, ili mpango huo uwe chombo muhimu cha kuanza kutekeleza Dira ya 2050.
Amesema muongozo huo unaainisha masuala muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika maandalizi ya mipango hiyo ili iwe na tija, ukizingatia malengo mapana ya kitaifa.
Aidha, alisema warsha hiyo imejadili pia Rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa kwanza katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambapo washiriki walitoa maoni yao kwa ajili ya kuboresha mpango huo.
“Kupitia maoni yao na utaratibu wa kawaida wa uandaaji wa nyaraka muhimu za kitaifa, tunapata mrejesho wa wadau, jambo ambalo ni msingi wa kupata mpango bora utakaokidhi matarajio ya Taifa,” alisema.
Dk. Msemwa aliongeza kuwa maoni hayo yatawezesha kuboresha maeneo ambayo hayakufanya vizuri, ili kupata muongozo na mpango wa maendeleo wenye ubora, unaoakisi fikra za wataalam na wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduma, Innocent Maduhu, aliishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo, akisisitiza kuwa hakuna maendeleo bila dira madhubuti.
Aliipongeza Serikali, hususan Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuzindua Dira ya Maendeleo 2050 ambayo alisema “ni wazi na inaongea yenyewe”.
Maduhu aliongeza kuwa endapo Dira hiyo itatekelezwa kama ilivyokusudiwa, hakuna Mtanzania atakayebaki katika hali ngumu ya maisha.

Naye Katibu Tawala Msaidizi wa Mipango na Uratibu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Edina Katakaiya, alisema warsha hiyo imewasaidia kupitia mpango wa utekelezaji wa miaka mitano pamoja na muongozo wake, na kwamba mpango huo “unaenda kuonekana kwa wananchi na sio kwa maneno”.




No comments:
Post a Comment