PROF. MKENDA ATAKA ELIMU ICHUKUE NAFASI YA KUWAANDAA VIJANA KUKABILIANA NA UKUAJI WA TEKNOLOJIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 27, 2025

PROF. MKENDA ATAKA ELIMU ICHUKUE NAFASI YA KUWAANDAA VIJANA KUKABILIANA NA UKUAJI WA TEKNOLOJIA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa katika kipindi hiki cha mageuzi ya teknolojia, ni muhimu elimu ichukue nafasi ya kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto pamoja na kutumia fursa za utandawazi, ambao sasa umegeuka kuwa mwelekeo wa dunia nzima.


Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo leo Novemba 27, 2025 jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa walimu wakuu wa shule za msingi Tanzania Bara (TAPSHA), ambapo amesema utandawazi ni fursa kubwa kwa mataifa yaliyojiandaa, lakini pia huibua changamoto zinazohitaji taifa kuwa na mfumo bora wa elimu unaomuwezesha kijana kuibuka na kutumia fursa hizo ipasavyo.


"Mageuzi ya elimu faida yake ni kizazi kijacho, na mwana siasa mwepesi atakwepa hilo atatafuta yale malaini laini, mageuzi ya elimu yanahitaji uvumilivu na sio suala la dharura na hilo ametuonesha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,"amesema. 


Aidha, amesema mageuzi makubwa yanayoendelea duniani yanabadilisha mfumo wa uzalishaji na utoaji huduma kwa kasi kubwa, na kuongeza tija katika uchumi. Amesema iwapo Tanzania haitajiandaa vyema kupitia elimu hususan ya Sayansi na Teknolojia, itaendelea kubaki mnunuzi wa bidhaa kutoka nje.

"Rais wetu alisema sababu nyingine ya mageuzi ya elimu ni huu mfumko mkubwa wa Sayansi na Teknolojia duniani ambao unarahisisha mambo mengi, utoaji wa huduma, uzalishaji wa bidhaa hata bei ya bidhaa inashuka lakini kama sisi hatukuweza kwenda kwa kasi hiyo ya Sayansi na Teknolojia hatutaweza kuzalisha bidhaa kwa bei ndogo watu watapenda kununua bidhaa kutoka nje, kwahiyo ule utandawazi ule utakuja tena kutugonga halafu hawa vijana walio wengi wanaokua kazi watakuwa hawana,"amesema. 


Ameongeza kuwa halmashauri zote nchini zinapaswa kubainisha maeneo ambako shule za msingi zitaongezewa madarasa ya sekondari ili kupunguza umbali unaowalazimu watoto kutembea kwenda kusoma ngazi hiyo.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAPSHA, Bi. Rehema Ramole, amemuomba Waziri kuhakikisha wakuu wa shule wanapatiwa mafunzo ya kutosha kuhusu mitaala iliyoboreshwa pamoja na kushirikishwa kwenye tathmini za mabadiliko ya mtaala mpya. 


Ameongeza kuwa lengo la TAPSHA ni kuwaunganisha wakuu wa shule za msingi nchini ili kushirikiana katika kutatua changamoto za kitaaluma, pamoja na kuwawezesha wanachama kupitia semina za uongozi na mikutano inayolenga kuboresha uwezo wao wa kiutawala.

No comments:

Post a Comment