TAKUKURU YAIMARISHA HUDUMA ZA WATOTO NJITI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 27, 2025

TAKUKURU YAIMARISHA HUDUMA ZA WATOTO NJITI



Na Mwandishi Wetu , DODOMA


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetoa mashine mbili za kuongezea joto watoto wanaozaliwa na uzito mdogo (njiti) ili kusaidia kukabiliana na wimbi la watoto wanaowasili kila mwezi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Hospitali hiyo inapokea takribani watoto njiti 60 kila mwezi, idadi ambayo ni kubwa kuliko uwezo wa kuwahudumia.

Akizungumza leo Novemba 27,2025, jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi mashine hizo, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Ernest Ibenzi, alisema msaada huo umekuja wakati muafaka kutokana na ongezeko la watoto wanaozaliwa njiti.

“Tunaishukuru sana TAKUKURU kwa kuleta mashine hizi. Wamekuwa sehemu ya familia ya General Hospital kutokana na ushirikiano wao katika mambo mbalimbali ya kitabibu,” alisema Dk. Ibenzi.

Aliongeza kuwa licha ya wingi wa watoto wanaozaliwa njiti, hospitali inaendelea kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanatunzwa ipasavyo hadi kufikia hatua ya kutoka hospitalini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Francis Chalamila, alisema mashine hizo ni sehemu ya mchango wa taasisi hiyo katika kusaidia huduma za afya nchini, hususan kwa watoto njiti.

Alisema wameamua kushirikiana na hospitali mbalimbali baada ya tafiti kubaini uhaba wa mashine hizo nchini.

“Mashine hizi ni mchango unaotokana na fedha zilizochangwa na watumishi wetu kutoka vitengo mbalimbali. Tunashukuru kwa ushirikiano, hadi Mganga Mkuu wa Mkoa amehudhuria hafla hii,” alisema Chalamila.

Aliongeza kuwa msaada huo ni njia ya kurejesha shukrani kwa wananchi kwa ushirikiano wanaotoa katika mapambano dhidi ya rushwa.

Naye Daktari Bingwa wa Watoto, Dk. Happy Kamongo, alisema watoto wanaozaliwa na uzito mdogo wapo katika hatari ya kupata manjano ambayo inaweza kusababisha matatizo ya ubongo, hivyo ni muhimu wazazi kuwapeleka hospitalini mapema.

Alisema watoto njiti hutunzwa hadi kufikia hatua salama ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.





No comments:

Post a Comment