
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imesema serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka na za kitaalamu kuhakikisha mvua zinazoendelea kunyesha nchini hazikatizi huduma za usafiri na usafirishaji, hususani katika maeneo yaliyoathirika na changamoto za kimazingira.
Akizungumza katika ziara ya kukagua hatua za utekelezaji wa miradi inayoboreshwa kukabiliana na mvua leo Jumamosi Novemba 22, 2025, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kuongeza uimara wa miundombinu ili kuzuia athari zinazoweza kusababishwa na mvua za msimu.
Mhandisi Besta alizungumza akiwa eneo la Mbande, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, ambako TANROADS imekamilisha uboreshaji wa kipande cha barabara kilichokuwa kikikumbwa na uharibifu wakati wa mvua, amesema mradi huo upo katika hatua za mwisho na wahandisi wa TANROADS pamoja na mkandarasi wanaendelea na ukamilishaji wake.
"Hivi sasa hakuna tena changamoto katika eneo la Mbande. Tumeboresha miundombinu ili kuhakikisha mvua haziathiri tena barabara hii," alisema.
Ameendelea kwa kusema kuwa, nchi imeathirika kwa viwango tofauti katika kipindi hiki cha mvua, ambapo baadhi ya barabara zimepata uharibifu katika mikoa ya Njombe (hasa barabara ya Itoni–Lusitu), Ruvuma, Mbeya, Arusha, Rukwa na Katavi ambapo ameeleza pia kwa baadhi ya maeneo, uharibifu unatokana na ujenzi unaoendelea.
Vilevile amesema TANROADS inaendesha kazi zake kwa kuzingatia Emergency Response Manual ambao ni mwongozo wa kitaalamu unaoelekeza hatua za kuchukua wakati wa dharura zinazosababishwa na mazingira.
Katika hatua nyingine, amewataka Mameneja wa TANROADS wa Mikoa yote nchini kuendelea kusimamia kwa umakini miradi na maeneo yao, si tu pale panapopata athari za mvua, bali hata maeneo ambayo bado hayajaathirika ili kuzuia uharibifu kabla haujatokea.
"Wananchi wasiwe na wasiwasi. Serikali iko kazini kupitia TANROADS. Tutaendelea kuhakikisha barabara zinapitika na usafirishaji wa watu, bidhaa na mazao unaendelea bila kukwama," alisisitiza.










No comments:
Post a Comment