
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amesema Serikali imetenga Shilingi bilioni 62 kwa ajili ya kutekeleza mikakati ya muda mfupi ya kuboresha huduma ya maji jijini Dodoma.
Aweso ameyasema hayo mbele ya Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA),ambapo amesema Serikali imeandaa mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na maeneo ya pembezoni.
Amesema kuwa uwekezaji huo wa awali wa Sh. bilioni 62 unalenga miradi ya haraka itakayoboreshwa kuhakikisha huduma ya maji inakuwa bora, ya uhakika na endelevu, sambamba na hadhi ya Dodoma kama Makao Makuu ya Nchi.
“Jiji la Dodoma ni Makao Makuu ya nchi. Ni wajibu wetu kuhakikisha huduma ya maji inakuwa bora na inayotabirika. Tutatumia fedha, nguvu na akili zetu kufanikisha lengo hili,” amesema Aweso.
Waziri Aweso pia amesisitiza kipaumbele cha Wizara kuwa ni kuboresha utoaji huduma, kuhakikisha malalamiko ya wananchi yanapungua, na kuondoa urasimu katika kushughulikia changamoto za wateja.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amewataka watumishi wa DUWASA kuheshimu Mkataba wa Huduma kwa Mteja, kupunguza upotevu wa maji ambao kwa sasa umefikia asilimia 32, na kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa kikamilifu.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA alibainisha kuwa mamlaka imeendelea kuimarika kiutendaji, ikiongeza makusanyo kutoka Sh. bilioni 1.5 hadi bilioni 2.8 kwa mwaka, kiasi kinachotumika kuboresha huduma kwa wananchi.




No comments:
Post a Comment