ULEGA AAGIZA MIRADI YA MIUNDOMBINU IKAMILIKE NDANI YA WIKI MBILI, ATOA ONYO KUHUSU UHARIBIFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 22, 2025

ULEGA AAGIZA MIRADI YA MIUNDOMBINU IKAMILIKE NDANI YA WIKI MBILI, ATOA ONYO KUHUSU UHARIBIFU


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza kukamilishwa kwa miradi ya maboresho ya miundombinu ya madaraja, barabara na maeneo ya maegesho wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, ndani ya kipindi kisichozidi majuma mawili ili kuwanusuru watumiaji wa barabara na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi.


Ulega ametoa maagizo hayo leo Novemba 22,2025 jijini Dodoma alipotembelea miradi ya maendeleo katika maeneo korofi ya Barqbara, ikiwemo Daraja na Tuta la Mbande, Mradi wa Dharura wa Ujenzi wa Madaraja na Tuta la Mtanana, Maegesho ya Magari Kibaigwa, pamoja na Mradi wa Dharura wa Ujenzi wa Madaraja na Tuta la Pandambili na Silwa.


Akizungumza na wananchi, Ulega amewataka kutunza miundombinu iliyopo na kuacha kushawishiwa kufanya vitendo vinavyopelekea uharibifu, akisisitiza kuwa serikali ipo tayari kusikiliza na kutatua changamoto zao bila kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa miundombinu.


“Jitahidini kutunza miundombinu. Yale yaliyotokea karibuni yametuchafua, na mna uwezo wa kufikisha changamoto zenu kupitia viongozi wenu. Serikali ipo tayari kusikiliza na kuzitatua. Msikubali kushawishiwa kufanya uharibifu,” amesema Ulega.


Aidha, Waziri Ulega amewataka wakandarasi wazawa wanaotekeleza miradi hiyo kufanya kazi kwa ubora, kasi na kwa kuzingatia viwango, akisema serikali ina maelekezo mahsusi ya kuwapa kazi wakandarasi waliothibitisha uwezo na uadilifu.



Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, amesema uchakavu wa makaravati ya zamani na wingi wa maji kutoka mikoa jirani ikiwemo Manyara kulisababisha athari kubwa katika eneo hilo, hivyo kufanya usanifu mpya ili kukidhi kiwango cha maji kinachopita.


“Eneo hili lilikuwa na makaravati ya chuma ambayo hayakuweza kuchukua wingi wa maji. Tumeongeza makaravati mapya na kuinua tuta la barabara kwa urefu wa kilomita 2.5, pamoja na kurudishia matabaka ya barabara hadi kufikia hatua ya kuweka lami,” amesema.


Amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi mzawa King’s Builders LTD, uliyoanza Novemba 15, 2024 na unatarajiwa kukamilika Desemba 25, 2025 kwa gharama ya shilingi bilioni 7.9, fedha za dharura za SEC chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.


Hadi sasa mradi umefikia asilimia 88, ambapo kazi kubwa iliyobaki ni uwekaji wa lami na samani za barabarani ikiwemo michoro, alama, na taa 50 zitakazowekwa ili kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara.


Mhandisi Zuhura amebainisha kuwa kuchelewa kupatikana kwa lami kulisababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli kwa takribani mwezi mmoja, lakini sasa ugumu huo umeondoka, na mkandarasi ameahidi kukamilisha kazi ya lami ndani ya wiki moja.








No comments:

Post a Comment