
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Katika juhudi za kuendeleza kutangaza fursa mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo wa uongezaji thaman madini ya vito na metali za thamani, Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kimefungua vituo maalum vya kutangaza fursa zilizopo kwenye mnyororo wa uongezaji thamani madini nchini katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) na katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Hayo yamebainishwa leo Novemba 7, 2025 na Mkuu wa Kituo hicho Mha. Ally Maganga wakati akielezea namna vituo hivyo vitakavyotangaza fursa mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo mzima wa thamani madini hususan kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.
Akielezea kuhusu faida zitakazopatikana kupitia vituo hivyo Mha. Maganga amesema kuwa, lengo kubwa la kufungua vituo hivyo ni kutangaza, kuelimisha, kuhamasisha, kukuza uelewa kwa jamii kuhusu shughuli zinazofanywa na TGC.
Sambamba na fursa za kimataifa, pia vituo hivyo vitafungua fursa za upatikanaji wa ajira na kuongeza shughuli za ujasiriamali kwa vijana mbalimbali wenye ujuzi katika uongezaji thaman madini hususan katika viwanda vya usonara.
Mha. Maganga amefafanua kuwa, mbali na fursa hizo, vituo hivyo vitahamasisha na kuvutia uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa madini itakayosaidia uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata madini ya vito na utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na rasilimali madini kama vile herein, pete, shanga , vinyago , mikufu na tuzo.
Akielezea kuhusu Utalii wa madini Mha. Maganga ameeleza kuwa, faida nyingine ni kukuza utalii wa madini kupitia watalii wanatoka na kuingia nchini kupitia kiwanja cha KIA na wageni watakaoshiriki mikutano ya kitaifa na kimataifa kupitia ukumbi wa AICC.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kati wa Madini (Broker) Jeremiah Kituyo ameipongeza TGC kwa kupanua wigo wa fursa za kibiashara utakaohamasisha ushirikiano mzuri kati ya Sekta Binafsi na Serikali hasa kwenye mnyororo wa uongezaji thaman madini ya vito na metali za thamani (precious metals) kama Sera ya Madini ya Mwaka 2009 inavyoelekeza.



No comments:
Post a Comment