
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Tume ya Utumishi wa Umma inatarajia kujadili na kutoa uamuzi kuhusu rufaa na malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa na watumishi wa umma kupitia Mkutano wake wa Pili wa mwaka, unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume, mkutano huo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria, utafanyika kuanzia Desemba 1 hadi 19, mwaka 2025 mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya mikutano yake ya mwaka wa fedha 2025/26.
Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso, amesema kwa mujibu wa kifungu cha 12(1)(d) na kifungu cha 27(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (Marejeo ya 2023), Tume imepewa mamlaka ya kupokea na kushughulikia rufaa na malalamiko kutoka kwa watumishi wa umma ambao hawajaridhishwa na maamuzi ya waajiri, mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu katika utumishi wa umma.
Amesema rufaa hizo ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki, uwazi na uwajibikaji vinazingatiwa katika usimamizi wa rasilimali watu serikalini.
Katika hatua nyingine, Tume hiyo imepanga kufanya ziara kwenye baadhi ya taasisi za Serikali zilizopo katika Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kutoa elimu kwa waajiri, mamlaka za ajira na nidhamu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika usimamizi na uendeshaji wa masuala ya rasilimali watu.



No comments:
Post a Comment