
Na Mwandishi Wetu, Manyara
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde (Mb), ametembelea na kushuhudia utekelezaji wa utafiti wa kina wa madini kwa kutumia teknolojia ya ndege nyuki (drone) katika Kata ya Basotu, Wilaya Hanang, mkoani Manyara. Utafiti huo wa jiofizikia unalenga kubainisha maeneo yenye hifadhi ya madini na kuongeza tija katika usimamizi wa rasilimali hiyo muhimu.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati akihutubia Bunge Oktoba 13, 2025 ambapo alitaja utafiti wa madini kama kipaumbele kwa mwaka 2025 - 2030 utakaopelekea kufikia angalau asilimia 50 ya utafiti wa kina wa madini nchini ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Mavunde amesema utafiti huo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Hanang na Mkoa wa Manyara kwa ujumla, kwani matokeo yake yanatarajiwa kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kuchochea utekelezaji wa miradi ya kijamii kupitia leseni za uchimbaji madini.
“Tunatarajia utafiti huu utaleta matokeo chanya yatakayobadilisha maisha ya wananchi. Serikali itaendelea kusimamia sekta hii ili iwe chachu ya maendeleo kwa wote,” amesema Mavunde.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mhe. Almish Hazal, amemshukuru Waziri Mavunde kwa kutembelea eneo la mradi huo na kuendelea kusisitiza umuhimu wa tafiti za madini katika wilaya yake pia, ameiomba Wizara ya Madini kuendeleza kasi hiyo katika maeneo mengine ya Hanang yenye uwezekano wa kuwa na madini.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Cobra Resources Ltd, *Bw. Amos Nzungu*, amempongeza Waziri Mavunde kwa ushirikiano na uzalendo anaouonesha kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya utafiti wa madini na kuahidi kukabidhi matokeo ya utafiti mara tu yatakapokamilika.
Kwa upande wa Meneja wa Kampuni ya SkyPM Solution inayofanya utafiti huo, Bw. Paul Madata amesema matumizi ya teknolojia ya ndege nyuki yamerahisisha na kuongeza ufanisi wa utafiti wa awali, kwani inaweza kupima hadi zaidi ya kilomita tatu chini ya uso wa ardhi kwa muda mfupi.
Awali, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Manyara, Mhandisi Godfrey Nyanda ametoa taarifa ya maendeleo ya sekta ya madini mkoani hapo, akibainisha kuwa hadi kufikia robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 (Julai–Oktoba), wamekusanya asilimia 35.21 ya lengo la makusanyo ya Shilingi Bilioni 2.2 lililopangwa kwa mwaka mzima.
“Tutaendelea kusimamia kikamilifu maagizo ya Mhe. Rais na ya Waziri wetu Mhe. Mavunde ili kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kukua na kuimarika hapa Manyara,” amesema Mha. Nyanda.





No comments:
Post a Comment