WAZIRI KIJAJI AIPA TANAPA MAELEKEZO MAHSUSI UHIFADHI WA WANYAMAPORI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 27, 2025

WAZIRI KIJAJI AIPA TANAPA MAELEKEZO MAHSUSI UHIFADHI WA WANYAMAPORI



Na Mwandishi Wetu, Arusha


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amelielekeza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuhakikisha kuwa ustawi na usalama wa wananchi unazingatiwa wakati wa kutekeleza majukumu ya uhifadhi wa wanyamapori, ili kulinda maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Dkt.Kijaji ameyasema hayo jijini Arusha katika kikao na Menejimenti ya TANAPA ikiwa ni sehemu ya ziara maalum ya mikakati ya kufuatilia na kujifunza utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi zilizo chini ya wizara kwa mujibu wa majukumu yao.

Amesisitiza kuwa dhana ya uhifadhi haiwezi kutenganishwa na utu wa mwananchi, sambamba na kuthamini kazi ngumu inayofanywa na askari na watumishi wanaotekeleza majukumu yao katika mazingira hatarishi ndani ya hifadhi.

“Hakikisheni kila uamuzi, kuanzia ngazi ya askari wa doria hadi maafisa, unazingatia utu, sheria na staha. Dumisheni mazingira bora ya kazi, motisha kwa askari na mawasiliano mazuri na jamii inayozunguka hifadhi, kwani wao ndiyo wadau wa kwanza wa uhifadhi,” amesema Dkt. Kijaji.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameitaka TANAPA kuimarisha doria za kisasa, kutumia intelejensia makini, drones, kamera za ufuatiliaji (GPS collars) ili kuongeza ufanisi katika kukabiliana na ujangili, biashara haramu ya nyara na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa.

Amesema kuwa katika safari ya kufikia lengo la kuvutia watalii milioni nane, TANAPA inapaswa kuboresha vivutio vya utalii vilivyopo, kuimarisha miundombinu ya hifadhi na kubuni mazao mapya ya utalii, hususan katika maeneo mapya yaliyohifadhiwa.

“Lazima tumsaidie Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ametufungulia milango kupitia Royal Tour. Ili kufikia malengo yetu, tuongeze nguvu katika Kanda ya Kusini, Magharibi na Mashariki ili kuongeza mapato kupitia utalii,” amesisitiza.


No comments:

Post a Comment