Mwandishi Wetu
Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amezieleza nchi za Afrika kwamba Tanzania iko tayari na imejipanga kimkakati kwa uwekezaji mkubwa wa uzalishaji wa dawa na teknoloajia mbalimbali za afya.
Ametoa hakikisho hilo leo Alhamisi, 27 Novemba 2025, mbele ya wajumbe wa Mkutano wa Mawaziri kuhusu Uzalishaji wa Ndani wa Dawa na Teknolojia barani Afrika unaoendelea nchini Algeria.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine unalenga kuimarisha sekta ya dawa na teknolojia ya afya barani Afrika kama ilivyoazimiwa wakati wa kikao cha 74 cha Shirika la Afya Duniani (WHO)- Kanda ya Afrika kilichofanyika Agosti 2024.
Baadhi ya nchi zinazoshiriki mkutano huo ni Uganda, Zimbabwe, Jamhuri ya Kongo, Niger, Chad, Jamhuri ya Kudemokrasia ya Kongo na Madagascar, Kenya,Ghana,Rwanda, Angola na Nigeria
Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zilizopewa kipaumbele katika mkutano huo kutokana na kuthamini uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na kihistoria wa nchi hizo mbili toka enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Waziri Mchengerwa aliyeongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo amesema anashiriki mkutano huo kwa unyenyekevu akiwaeleza Tanzania imedhihirisha kwamba inaweza kuwa mwenyeji Afrika kwa utengenezaji wa dawa wa kiwango cha duni.
‘’Leo, tunakutana wakati muhimu kwa bara letu, wakati ambao unahitaji ujasiri, maono na umoja wa madhumuni. Maamuzi tunayofanya hapa Algiers, yataamua usalama wa afya na uhuru wa kiuchumi wa Afrika kwa vizazi vijavyo,’’ amesema Waziri Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa amesema anashiriki mkutano huo ikiwa ni wiki ya pili tangu Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipomwamini na kumteua kuwa Waziri wa Afya.
Amewaeleza katika muda mchache usiozidi wiki mbili tangu alipoapishwa, ameweka wazi mkakati wa kuvutia wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye viwanda vya utengenezaji dawa na vifaa tiba.
Amesema ametoa waraka mahsusi unaoanzisha utekelezaji wa mkakati wa kuendeleza viwanda vya dawa na bidhaa za afya nchini Tanzania. Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya kwa uhakika ndani ya Tanzania.
Aidha, amesema Serikali inataka kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa sekta binafsi katika viwanda vya dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa nyingine za afya pamoja na kuiongezea Bohari ya Dawa (MSD) uwezo wa kununua, kuzalisha na kusambaza bidhaa hizo kwa ufanisi.
Waziri Mchengerwa amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba lengo ni kujiweka Tanzania kama kipaumbele kwa uwekezaji wa dawa unaoendana na viwango vya WHO, kushirikiana kimkakati na watengenezaji kwa ajili ya uhamishaji wa teknolojia, biashara za pamoja, na mikataba ya usambazaji ya pande mbili na kusaini makubaliano ya ushirikiano wa udhibiti kati ya TMDA na ANPP.
Amesema hatua ya kuzalisha dawa ndani ya nchi ni mkakati wa uchumi, usalama na uhuru ambapo utazalisha ajira, kupunguza matumizi ya nje na kuhakikisha Afrika haitakiwi tena kuwa ya mwisho duniani hususan wakati wa majanga kama ilivyokuwa wakati wa ugonjwa wa COVID-19.
Amesema kwa kipindi kirefu mifumo ya afya ya Afrika imekuwa ikitegemea zaidi uagizaji wa nje wa dawa, chanjo, vifaa vya uchunguzi, na teknolojia.
‘’COVID-19 ilitufundisha kwa uchungu kuwa utegemezi ni udhaifu. Lakini leo, tunachagua njia nyingine. Tunachagua kujitegemea, uvumbuzi na uwezo wetu kama Afrika,’’ amesema Waziri Mchengerwa.


No comments:
Post a Comment