WAZIRI NANAUKA ATAKA VIJANA WASIKILIZWE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 25, 2025

WAZIRI NANAUKA ATAKA VIJANA WASIKILIZWE



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka leo Novemba 25, 2025 amewasili mkoani Songwe kwa lengo la ziara ya kukutana na kuzungumza na vijana kuhusu masuala mbalimbali ya ustawi wa kundi hilo ikiwemo shughuli za Ajira, Uwezeshwaji kiuchumi, Elimu, Afya na Miundombinu kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Waziri Nanauka ametembelea kwenye vijiwe pamoja na miradi ya vijana katika eneo la Sogea stendi, Kilimanjaro, Kisimani, Stendi ya zamani ya Majengo na Mpemba.

Akizungumza mara baada ya kukutana na vijana hao amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanzisha Wizara maalumu ya Maendeleo ya Vijana nchini ili kuratibu na kusimamia kwa umakini masuala yote yanayohusu vijana ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zao kwa ufanisi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Waziri Nanauka alieleza falsafa tatu zinazoongoza Wizara hiyo kuwa ni Kasi ya kusikiliza na kutekeleza mawazo na ushauri wa Vijana, pili kuwafikia vijana walipo na kuwasikiliza ambapo viongozi wote wa Mikoa na Wilaya watafanya hivyo pia na tatu kuwekeza kwenye matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo Wizara itaanzisha mfumo maalum kuwezesha Vijana kufikisha mawazo na mchango ikiwemo changamoto zao ili Serikali ichukue hatua za kutatua kwa haraka.

Kwa upande mwengine, Vijana wa Boda Boda, Bajaji na wafanyabiashara wa Soko la Majengo Wilaya ya Momba wameomba viongozi walioteuliwa na Rais wamshauri Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa hekima na uzalendo ili nchi yetu itambue mahitaji na mawazo ya vijana.

Mara baada ya kuwasili katika mkoa huo, Waziri Nanauka alipokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Jabiru Makame ambaye alimpa taarifa juu ya hali ya maendeleo ya Mikoa huo.

Waziri Nanauka ameanza ziara kukutana na kujadiliana na Vijana ili kuweza kusikia mawazo yao kuhusu mustakabali wa Taifa hatua itakayochangia Serikali kuweka mipango mahsusi kwa ajili ya Maendeleo ya Vijana.


No comments:

Post a Comment