LESENI 73 ZA MADINI ZAFUTWA:“Sitawavumilia wanaozikalia bila kuziendeleza,” – Waziri Mavunde - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 25, 2025

LESENI 73 ZA MADINI ZAFUTWA:“Sitawavumilia wanaozikalia bila kuziendeleza,” – Waziri Mavunde




Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Wizara ya Madini imezifutia leseni 73 za madini baada ya wamiliki wake kushindwa kurekebisha makosa yaliyobainishwa na Tume ya Madini katika ukaguzi wake wa hivi karibuni.

Akizungumza mbele ya wanahabari leo Novemba 25,2025 jijini Dodoma , Waziri wa Madini, Antony Mavunde, alisema hatua hiyo ni sehemu ya msimamo wa serikali kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya taifa.

"Ninaiagiza Tume ya Madini kufuta jumla ya leseni 73 ambazo wamiliki wake wameshindwa kurekebisha makosa. Sitawavumilia watu wanaochukua leseni na kukaa nazo bila kuziendeleza," alisema Waziri Mavunde.

Kwa mujibu wa Waziri, Tume ya Madini ilitoa Hati za Makosa kwa leseni 205, ikijumuisha leseni 110 za utafiti wa madini na leseni 95 za uchimbaji mkubwa na wa kati. Baada ya kutakiwa kurekebisha dosari hizo, baadhi ya wamiliki walikidhi matakwa, huku wengine wakishindwa kufanya hivyo.

Miongoni mwa waliotelekezwa na hatua za marekebisho ni wamiliki wa leseni 44 za utafiti wa madini pamoja na wamiliki wa leseni 29 za uchimbaji wa kati, ambao wote walishindwa kurekebisha makosa yao kwa mujibu wa masharti ya sheria.

Waziri Mavunde aliwataka wamiliki wote wa leseni za madini kuhakikisha wanazingatia masharti na wajibu wa umiliki wa leseni zao, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote anayekiuka sheria.

Aidha, amewaalika wawekezaji wenye nia ya dhati—wadogo kwa wakubwa—kuwasilisha maombi ya leseni katika maeneo ya wazi, akiahidi kuwa Wizara itaharakisha mchakato wa upatikanaji wa leseni kwa wakati.

Mavunde ametoa wito kwa wawekezaji wote kutekeleza matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, huku Wizara ikiendelea kutoa ushirikiano kwa wote wanaotaka kufanya uwekezaji wenye tija katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment