Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yazindua kamati mpya ya Mifumo ya Malipo - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, December 3, 2025

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yazindua kamati mpya ya Mifumo ya Malipo

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua Kamati mpya ya Mifumo ya Malipo yenye lengo la kuimarisha uratibu, utawala, na ukuzaji wa mifumo ya kitaifa ya malipo. Kamati hiyo ilizinduliwa rasmi na Naibu Gavana, Bi. Sauda Kassim Msemo, katika hafla iliyofanyika Benki Kuu jijini Dar es Salaam Desemba 2,2025.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Bi. Msemo alisema kuanzishwa kwa Kamati hiyo ni hatua muhimu katika jitihada za nchi kujenga mazingira thabiti, bunifu na jumuishi ya mifumo ya malipo.


Naibu Gavana Bi.Msemo amebainisha kuwa, kwa kipindi cha miaka kadhaa, mifumo ya malipo nchini Tanzania imeendelea kukua na kupanuka kupitia hatua muhimu za kimaendeleo, ikiwemo kuanzishwa kwa mifumo kama ECH mwaka 2001, TISS mwaka 2004, TACH mwaka 2015, na Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Hapo (TIPS) mwaka 2021.

Bi. Msemo amesisitiza kuwa,kamati hiyo itakuwa jukwaa muhimu la kuleta ulinganifu wa kiutendaji katika sekta nzima.

Kamati hiyo inatarajiwa kutoa ushauri kwa Benki Kuu kuhusu mwelekeo wa kimkakati wa mifumo ya malipo nchini, kusaidia kutatua migogoro kati ya watumiaji wa mifumo ya malipo inayoendeshwa na benki, na kushirikiana na wadau katika kupitia na kuweka viwango na kanuni zinazosimamia mifumo ya malipo.

Katika hafla hiyo, wajumbe walipitia Hati ya Utendaji ya Kamati inayofafanua muundo wa utawala, majukumu, na taratibu za utendaji.

Hati hiyo itakuwa mwongozo mkuu katika kuhakikisha uwazi, uwajibikaji, na ufanisi wa kazi za Kamati hiyo mara itakapoanza kutekelezwa kikamilifu.

Naibu Gavana amewahimiza wajumbe kuchukua umiliki kamili wa kamati hiyo, akisisitiza kuwa uzoefu wao wa kiutendaji na uelewa wa kina wa sekta ni muhimu katika kuimarisha mifumo ya malipo nchini.

Ameongeza kuwa, kupitia ushirikiano wa pamoja, Tanzania inaweza kuwa na mifumo ya malipo iliyo jumuishi, salama, yenye ufanisi, inayoingiliana na inayoendana na viwango vya kimataifa.

Kamati hiyo inaundwa na wadau kutoka benki, taasisi zinazotoa huduma za pesa kidijitali, kampuni za mawasiliano ya simu pamoja na kampuni za teknolojia ya fedha.

No comments:

Post a Comment