
Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imefanya ziara ya kikazi katika miradi ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga - UWASA), Disemba 15, 2025, na kusisitiza umuhimu wa utoaji wa zabuni kwa vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Akizungumza baada ya kutembelea miradi hiyo na kusikiliza wasilisho kutoka Menejimenti ya Tanga - UWASA, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Prof. Leonada Mwagike, ameipongeza Mamlaka hiyo kwa utekelezaji mzuri wa miradi, huku akiitaka kuendelea kutoa kipaumbele kwa makampuni ya ndani ya nchi pamoja na vikundi vya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Miradi waliyoitembelea ni pamoja na mradi wa kuchakata na kutibu Maji wa Moe na Mradi wa Maji wa Mabayani, ambayo yote iko kwenye hatua za michakato ya ujenzi.
Prof. Mwagike amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 inatoa upendeleo maalum kwa makampuni ya ndani ya nchi ikilinganishwa na makampuni ya nje, ikiwemo kuweka kikomo cha zabuni za hadi Shilingi bilioni 50 kushindaniwa na makampuni ya ndani pekee.
Hivyo, ameitaka Tanga - UWASA kuendelea kutoa fursa kwa Watanzania, na pale ambapo zabuni zinatolewa kwa makampuni ya kigeni kutokana na mahitaji ya kiufundi au uwezo wa mtaji, makampuni ya ndani yashirikishwe ili nayo yaweze kujengewa uwezo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa taasisi za umma kuendelea kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki - NeST, ambao sasa umefikia hatua ya usimamizi wa mikataba (e-contract management) na malipo kwa njia ya kielektroniki (e-payment). Hatua hiyo inasaidia kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ubora na kwa wakati, pamoja na kuwahakikishia wazabuni malipo kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, amesisitiza umuhimu wa kutoa zabuni kwa vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, na kueleza kuwa kundi maalum haimaanishi kuwa ni kundi dhaifu kiutendaji, bali ni kundi lenye uwezo wa kutekeleza miradi linapopimwa na kuwa na vigezo husika, lakini mara kadhaa huwa na changamoto ya kutokuwa na uwezo mkubwa wa mtaji.
Ameeleza kuwa makundi hayo yanapaswa kuhamasishwa kuungana katika vikundi ili kuongeza nguvu ya pamoja na uwezo wa kutekeleza zabuni mbalimbali, ikiwemo zabuni za kiufundi kwani zabuni zao zinaweza kufikia Shilingi Milioni Mia Tano.
“Tunaona bado kuna dhana kuwa makundi maalum yanapaswa kupewa zabuni ndogo-ndogo au zisizo za kiufundi tu. Dhana hii sio sahihi. Vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu wana uwezo wa kutekeleza zabuni hata za kiufundi, ili mradi tu wakidhi vigezo. Ni vile hawana nguvu kubwa kama makampuni, ndiyo maana tunasisitiza waungane ili wawe na nguvu ya pamoja,” amesema Bw. Simba.
Ameongeza kuwa ni muhimu kuhakikisha asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi wa umma inatengwa kwa ajili ya makundi maalum na wanapewa.
Aidha, hata katika zabuni zinazotolewa kwa wazabuni wakubwa, inaweza kuwekwa masharti ya sub-contract ili sehemu ya kazi itolewe kwa vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kifedha na kitaalamu.
Bw. Simba pia ameipongeza Tanga UWASA kwa ubunifu wa kuanzisha chanzo cha mapato kupitia hati fungani ya kijani (Green Bond), akieleza kuwa Mamlaka hiyo ni miongoni mwa Mamlaka za Maji zinazoongoza kwa mafanikio katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuzingatia taratibu za utoaji wa zabuni na kuhakikisha ubora wa miradi yote inayotekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Tuhakikishe tunapata thamani halisi ya fedha katika kila mradi, sambamba na kuhakikisha ubora wa miradi yetu unaakisi matarajio ya wananchi katika kutatua changamoto zao na kuleta maendeleo,” amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tanga -UWASA, Dkt. Fungo Ally Fungo, ameishukuru PPRA kwa kufanya ziara hiyo ya kikazi, akieleza kuwa imewasaidia kukumbushwa maeneo m
uhimu ya kuzingatia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ameahidi kuwa Tanga UWASA itaendelea kushirikiana kwa karibu na PPRA ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi unazingatia kikamilifu Sheria ya Ununuzi wa Umma na kanuni zake.




No comments:
Post a Comment