
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema Bwawa la Maji la Kidunda linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha hadi lita bilioni 20 za maji kwa siku kwa ajili ya huduma ya majisafi na salama. Amesema mradi huo utatoa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upungufu wa maji inayolikabili Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya Pwani, hususan inayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Aweso ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro, mradi wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 329 unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Amesema nchi nyingi duniani kwa sasa zinakabiliwa na changamoto ya ukame inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo pia imeanza kuathiri Tanzania.
Kutokana na hali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliielekeza Wizara ya Maji kuchukua hatua za haraka na za muda mrefu ili kukabiliana na changamoto hiyo.
“Wizara ya Maji tuliweka mkakati wa muda mfupi jijini Dar es Salaam kwa kuchimba visima vitano vilivyogharimu takribani Shilingi bilioni 23.6, sanjari na mkakati wa muda mrefu wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro pamoja na mpango wa kutumia maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani ili kuongeza uzalishaji wa maji,” Waziri Aweso amefafanua.
Amesema kwa sasa mahitaji ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam ni takribani lita milioni 534 kwa siku, ilhali changamoto ya ukame ikiathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma ya maji.
Kutokana na hali hiyo Serikali imetoa kipaumbele kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda, ambao hadi sasa umefikia asilimia 40 ya utekelezaji na utakuwa ni suluhisho la kudumu kwa huduma ya maji kwa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Waziri Aweso ameongeza kuwa kazi nyingi za kiufundi za mradi huo zimekamilika, na kazi kubwa iliyosalia ni kukamilisha ujenzi wa mageti ya bwawa. Amesisitiza kuwa ifikapo mwezi Aprili, 2026, maji ya Mto Ruvu yataanza kuingia kwenye bwawa hilo.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amesema Serikali itaendelea na mkakati wa kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji katika maeneo mbalimbali nchini ili kuvuna maji ya mvua na kuyatumia katika nyakati za kiangazi.
Waziri Aweso ameambatana Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, pamoja na Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro katika ziara yake hiyo ya kimkakati.
Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira katika chanzo cha Mto Ruvu, kina cha maji cha mto huo kimekuwa kikishuka hususan wakati wa kiangazi, hali inayosababisha mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kushindwa kusukuma maji kwa kiwango kinachohitajika na hivyo kuathiri huduma ya maji kwa wananchi.
Mradi wa Bwawa la Kidunda ni muhimu kwa kuwa utawezesha kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi wanaotarajiwa kuongezeka na kufikia idadi ya watu 11,387,753 ifikapo mwaka 2032, ambapo mahitaji ya maji yanakadiriwa kufikia zaidi ya lita bilioni 1.028 kwa siku. Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi kutoka kampuni ya Sino Hydro Corporation ya nchini China.
Bwawa la Kidunda, litakalokuwa na ujazo wa lita bilioni 190, litawezesha mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya lita milioni 466 kwa siku, kufanya kazi katika majira yote ya mwaka na hivyo kuondoa upungufu wa maji wakati wa kiangazi.
Mitambo hiyo inahudumia zaidi ya asilimia 80 ya eneo lote la huduma la DAWASA.

No comments:
Post a Comment