
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, ameanza utekelezaji wa ahadi yake ya kutatua changamoto ya barabara iliyowasilishwa na mwananchi wa Shunu ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT–Wazalendo wilayani Kahama, Abas Omari, wakati alipokutana na vijana katika sherehe za Krismasi maarufu kama Pilau la Wana.
Katika sherehe hizo, DC Nkinda aliahidi kutembelea eneo husika ili kujionea ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua stahiki, Leo, ametimiza ahadi hiyo kwa kutembelea barabara yenye changamoto katika Mtaa wa Hongwa, Kata ya Nyahanga, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, inayounganisha eneo la Shunu na eneo la viwanda la Zongomela maarufu Dodoma.
Akiwa katika ziara hiyo, DC Nkinda amejionea adha inayowakabili wananchi wanaoutumia barabara hiyo, hususan wafanyabiashara na wafanyakazi wa viwanda vidogo vidogo zongonela, Kutokana na umuhimu wake kiuchumi, ameagiza mkandarasi anayetekeleza mradi huo Prinax investment limited kuhakikisha anakamilisha ujenzi kwa wakati uliopangwa ili kuondoa kero kwa wananchi na kurahisisha shughuli za uzalishaji na biashara.

Akizungumza kuhusu hatua za utekelezaji wa mradi, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), mhandisi Juma Masola, ameahidi kumsimamia kwa ukaribu mkandarasi anayetekeleza mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, hivyo kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea bila vikwazo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nyahanga, Mheshimiwa Josephina Kilimba, amwtaja barabara nyingine korofi zinazohitaji matengenezo ya dharura, ikiwemo barabara ya Vatikani iliyopo Mtaa wa Lugela huku akisisitiza umuhimu wa hatua za haraka ili kuboresha miundombinu na kuongeza ustawi wa wananchi.
Wananchi wa eneo hilo wamepongeza jitihada za Serikali ya Wilaya ya Kahama kwa kuanza kuchukua hatua za vitendo katika kutatua changamoto za barabara, wakieleza matumaini kuwa maboresho hayo yataongeza fursa za kiuchumi na kuboresha maisha yao kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment