DC NYAMWESE: MADIWANI HANDENI MJI ONGEZENI UBUNIFU WA VYANZO VYA MAPATO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, December 5, 2025

DC NYAMWESE: MADIWANI HANDENI MJI ONGEZENI UBUNIFU WA VYANZO VYA MAPATO



Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese,akizungumza wakati akifungua Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Handeni lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.


Na Mwandishi Wetu, Handeni TC


Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, ametoa wito kwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji Handeni kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi katika kubuni vyanzo vipya vya mapato, sambamba na kuimarisha umoja, amani na uzalendo katika maeneo yao ya utawala.

Wito huo umetolewa katika ufunguzi wa Baraza la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, muda mfupi baada ya madiwani hao kuapishwa rasmi kuanza kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Nyamwese amewataka madiwani kuhakikisha wanakuwa chachu ya amani na utulivu, akisisitiza kuwa misingi hiyo ni nguzo muhimu kwa ustawi wa jamii na utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Amebainisha kuwa madiwani wana wajibu mkubwa wa kushirikiana kikamilifu na Mkurugenzi wa Halmashauri katika kubuni vyanzo vipya na endelevu vya mapato vitakavyoongeza uwezo wa Serikali ya Mtaa kusimamia na kutekeleza miradi ya wananchi.

Aidha, ameeleza kuwa kuimarisha ukusanyaji mapato na kusimamia miradi ya kimkakati kutasaidia kupunguza utegemezi na kuongeza kasi ya maendeleo ya Halmashauri.

“Madiwani mna wajibu wa kuhakikisha ushirikiano baina ya watendaji na wananchi unaongezeka ili kufanikisha malengo ya pamoja ya maendeleo,” amesisitiza.

No comments:

Post a Comment