HAKUNA MTOTO ATAKAYEZUIWA KUSOMA KWA KUKOSA SARE ZA SHULE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 30, 2025

HAKUNA MTOTO ATAKAYEZUIWA KUSOMA KWA KUKOSA SARE ZA SHULE



Na Angela Msimbira, Dar es Salaam


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha hakuna mtoto anayezuiwa kuanza au kuendelea na masomo kwa sababu ya kukosa sare, wakati shule zote nchini zikitarajiwa kufunguliwa rasmi Januari 13, 2025.

Prof. Shemdoe amesema kuwa agizo hilo linapaswa kusimamiwa kikamilifu katika maeneo yote ya nchi ili kuhakikisha kila mtoto anapokelewa shuleni bila masharti yanayokiuka miongozo na sera za elimu.

Amesisitiza kuwa mara mtoto anapopokelewa shuleni, masuala mengine ikiwemo sare, yataendelea kushughulikiwa akiwa tayari anaendelea na masomo, hatua itakayosaidia kuondoa vikwazo vinavyowafanya baadhi ya watoto kukosa haki yao ya msingi ya elimu.

Aidha, Prof. Shemdoe amekemea tabia ya baadhi ya shule za Serikali kuweka michango mingi kwa wazazi, ikiwemo kuwalazimisha kununua sare shuleni, akieleza kuwa hatua hiyo ni kinyume na taratibu na miongozo ya Serikali.

Ameelekeza walimu wakuu, walimu na viongozi wa shule kusoma, kuelewa na kuzingatia miongozo ya elimu iliyopo, pamoja na kutoa elimu sahihi kwa wazazi na walezi ili kuondoa sintofahamu zisizo za lazima.

“Lengo la Serikali ni kuona watoto wote wanakwenda shule bila vikwazo vyovyote, na kuhakikisha hakuna mtoto anayenyimwa haki yake ya elimu kwa sababu ya changamoto za kiuchumi au maamuzi yasiyo sahihi,” amesisitiza Prof. Shemdoe.




No comments:

Post a Comment