HAYA HAPA MAJUKUMU SITA YA TUME YA UCHUNGUZI WA MATUKIO YA UVUNJIFU WA AMANI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 1, 2025

HAYA HAPA MAJUKUMU SITA YA TUME YA UCHUNGUZI WA MATUKIO YA UVUNJIFU WA AMANI.



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunji wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, Jaji Mstaafu Mohammed Chande Othman, leo amekutana na wahariri wa vyombo vya habari na kutoa ufafanuzi kuhusu majukumu na maeneo ya uchunguzi ambayo tume yake itayashughulikia.

Akizungumza mbele ya Wahariri leo Disemba 1,2025 jijini Dar es Salaam , Jaji Othman ameeleza kuwa tume imekabidhiwa majukumu makuu sita yanayolenga kubaini chanzo, nia, athari na hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na machafuko yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, tume itachunguza:Chanzo halisi na kiini cha tatizo wakati na baada ya Uchaguzi, Lengo lililokusudiwa na waliopanga au kushiriki katika matukio ya uvunjifu wa amani, Mazingira ya matukio, ikiwa ni pamoja na vifo, majeruhi na madhara ya kijamii na kiuchumi, Mazingira na hatua zilizochukuliwa na serikali, vyombo vyake na taasisi nyingine katika kukabiliana na matukio Hayo, Mapendekezo ya maeneo ya kuimarishwa katika uwajibikaji, utawala bora, haki za binadamu, utawala wa sheria na mifumo ya majadiliano ya kitaifa ili kuzuia machafuko kutokea tena na masuala mengine yoyote muhimu ambayo tume itaona yanaendana na majukumu yake.

Jaji Othman amesisitiza kuwa tume ina uhuru wa kutafsiri hadidu zake za rejea na itafanya kazi yake kwa kuzingatia Sheria ya Tume ya Uchunguzi pamoja na taratibu itakazoweka chini ya mwongozo wa sheria hiyo.

Amesema uchunguzi utafanyika zaidi katika maeneo yaliyokumbwa kwa kiasi kikubwa na machafuko ili kubaini aina ya matukio, chanzo chake, madhara pamoja na hatua zilizochukuliwa katika kudhibiti hali hiyo.

“Tume itawaalika watu mbalimbali kwa mahojiano ili kupata taarifa sahihi na za kweli. Tunawaomba Watanzania kushirikiana kwa kutoa taarifa zitakazoiwezesha tume kufanikisha kazi yake,” alisema Jaji Othman.

Ameongeza kuwa tume itatumia mbinu mbalimbali kukusanya taarifa ikiwemo mapitio ya nyaraka, mahojiano ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao, dodoso la mtandaoni, barua pepe, barua za kawaida, ujumbe mfupi, mijadala ya makundi na ushauri wa kitaalamu.

Miongoni mwa wadau muhimu watakaoshirikishwa ni waathirika wa machafuko, watuhumiwa, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wasimamizi wa uchaguzi, Tume Huru ya Uchaguzi, viongozi wa dini, bodaboda, wamachinga, wafanyabiashara, wajasiriamali, sekta binafsi, wataalamu, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na waandishi wa habari.

Jaji Othman amebainisha kuwa Watanzania wengi wanatarajia uchunguzi wa wazi, wa kina na wenye uaminifu, akisema tume inakusudia kufanya mikutano ya hadhara na kukusanya ushahidi utakaoisaidia nchi kuelewa kilichotokea.

“Pamoja na maumivu tuliyoyapitia, majibu ya mambo mengi yapo kwetu wenyewe. Tusaidiane kuyatafuta ili yawe msingi wa majadiliano na maridhiano ya kitaifa,” alihitimisha.

No comments:

Post a Comment