KATIBU MKUU UJENZI AAGIZA TANROADS KUPUNGUZA MSONGAMANO JIJINI DAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, December 6, 2025

KATIBU MKUU UJENZI AAGIZA TANROADS KUPUNGUZA MSONGAMANO JIJINI DAR



Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, ameuelekeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kufungua kwa muda barabara zote za makutano katika maeneo yanayotekelezwa miradi ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) ili kupunguza msongamano wakati ujenzi ukiendelea.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo jijini Dar es Salaam, Balozi Amour alisema hatua hiyo imelenga kupunguza msongamano wa magari kuelekea kipindi cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, ambacho kwa kawaida huongeza idadi ya watu na magari jijini humo.

“Tumeona njia ya haraka ya kupunguza msongamano katika kipindi hiki ni kufungua barabara za makutano wakati tukisubiri ujenzi wa kudumu wa barabara hizo unaoendelea, ikiwemo ule wa BRT”.

Aidha, ameelekeza wakandarasi wote kuhakikisha kuwa barabara za michepuko zinapitika na ziko katika hali nzuri. Amesema kuwa mkandarasi anayejenga kipande cha barabara ya Mwenge–Tegeta ameahidi kuweka lami ya muda katika barabara ya mchepuko ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.

Balozi Amour ameongeza kuwa ili kupunguza malalamiko yanayotokana na msongamano unaosababishwa na utekelezaji wa mradi wa BRT, TANROADS itatoa taarifa za mara kwa mara ili kuwasaidia watumiaji wa barabara kujua njia mbadala yakutumia wakati wa kwenda na kurudi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Ametoa wito kwa wananchi kufuata sheria za usalama barabarani, ikiwemo kuzingatia vibao vya muda vitakavyowekwa katika maeneo husika.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema tayari wameanza kuyafanyia kazi maelekezo ya Katibu Mkuu na wamewaelekeza baadhi ya wakandarasi kuanza kufungua barabara hizo.





No comments:

Post a Comment