MIAKA 64 YA UHURU : TBN YATOA WITO WA AMANI NA UJENZI WA TAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 9, 2025

MIAKA 64 YA UHURU : TBN YATOA WITO WA AMANI NA UJENZI WA TAIFA



Tanzania Bloggers Network (TBN) imewataka Watanzania kuendeleza misingi ya amani, umoja na mshikamano wakati Taifa linaadhimisha miaka 64 ya Uhuru tangu kupatikana kwake mwaka 1961.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wake, Beda Msimbe, TBN imesema maadhimisho ya mwaka huu yanapaswa kutumika kama fursa ya kutafakari safari ya Taifa, mafanikio yaliyopatikana na wajibu wa kizazi kilichopo katika kuendeleza misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa.

Msimbe amesema zawadi ya Uhuru aliyoachiwa Taifa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inaambatana na wajibu wa kujitegemea, akilinukuu tamko maarufu la Nyerere kuwa:
“Uhuru hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea. Hatuwezi kuitwa huru kama tunategemea wengine kutupatia mahitaji yetu ya kimsingi.”

Amesema mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka 64 yanatokana na utulivu na mshikamano uliojengwa kwa muda mrefu, akionya kuwa misingi hiyo inaweza kutoweka endapo chuki, uchochezi na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yataachwa yaendelee.

Akirejea maneno ya Rais mstaafu Benjamin William Mkapa aliyewahi kusisitiza kuwa “Amani si kitu cha asili; tunahitaji kuilinda kila siku kwa sababu bila amani hakuna maendeleo,” TBN imetoa wito kwa Watanzania kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Aidha, Msimbe ametaja busara za Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyekumbusha kuwa “Kila utawala una zama zake na kila kiongozi ana mchango wake katika ujenzi wa Taifa,” akisema kauli hiyo inathibitisha umuhimu wa kuunga mkono juhudi za serikali ya sasa.

Katika awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, TBN imesema Tanzania inaendelea kusimamia falsafa ya 4R  Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding  ikilenga kuimarisha maridhiano, mageuzi, uimara wa kiuchumi na kuijenga Tanzania inayowapa matumaini wananchi wote.

TBN imewataka wananchi kutumia uhuru na majukwaa ya mawasiliano kwa lengo la kujenga Taifa, badala ya kuchochea migawanyiko, ikisisitiza kuwa ulinzi wa amani ni wajibu wa kila Mtanzania.


“Tanzania Kwanza — Kazi, Utu na Mshikamano. Tusonge mbele,” imesema taarifa hiyo, huku TBN ikiwatakia Watanzania maadhimisho mema ya miaka 64 ya Uhuru.

No comments:

Post a Comment