NMB YATOA MILIONI 500 KUSAIDIA MATIBABU YA MOYO YA WATOTO 125 NCHINI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 2, 2025

NMB YATOA MILIONI 500 KUSAIDIA MATIBABU YA MOYO YA WATOTO 125 NCHINI.



Benki ya NMB tayari imetoa nusu ya TZS bilioni 1 ilizoahidi mwaka jana kwa ajili ya kuiwezesha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kutoa matibabu ya moyo ya watoto 250 katika kipindi cha miaka minne, hatua ambayo imesaidia kubadili maisha ya familia zisizojiweza nchini.

Ahadi hiyo, iliyotolewa tarehe 2 Novemba mwaka jana, inalenga kugharamia upasuaji na matibabu ya watoto wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo na matatizo mengine ya mfumo wa moyo, hususan wale wanaotoka katika familia zenye kipato duni.

Jana, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, aliongoza ujumbe wa maafisa waandamizi wa benki hiyo kutembelea JKCI, ambapo alitangaza kuwa benki hiyo imeshatoa TZS milioni 500 ambayo ni sawa na nusu ya ahadi yote.

Kwa mujibu wa Bi Zaipuna, kiasi hicho kimesaidia kuwezesha upasuaji na matibabu ya moyo ya watoto 125.

“Tunawashukuru sana JKCI kwa kazi yao ya kipekee ya kufanya upasuaji huuna tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu ili kuwasaidia Watanzania hasa familia zisizojiweza kupata matibabu na huduma stahiki,” alsiema.

Aliongeza kuwa kiasi kingine cha TZS milioni 250 kitatolewa Januari mwakani ili kuhakikisha mchakato wa matibabu magonjwa ya moyo ya ya watoto unaoendelea na kufanyika bila kukwama.

Bi Zaipuna pia alisisitiza kuwa msaada wa NMB hauishii kwenye fedha pekee.

Benki hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na JKCI, Heart Team Africa Foundation, na Global Medicare ili kupanua wigo wa huduma, kuongeza kasi ya upasuaji, na kuimarisha miundombinu ya huduma za moyo kwa watoto.

Moja ya mapendekezo na maombi aliyoyapokea ni suala la kuanzisha “Recovery House” — kituo maalum cha kuwapokea watoto wanaosubiri upasuaji au kuendelea na matibabu — ambacho kitasaidia kupunguza mzigo wa kifedha na changamoto za makaazi kwa familia kutoka maeneo ya mbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, alisema NMB imekuwa mdau namba moja katika kusaidia familia zisizojiweza kupata huduma muhimu za moyo.Bingwa huyo wa magonjwa ya moyo alibainisha kuwa mchango wa benki hiyoumeongeza ufanisi wa huduma, kupunguza muda wa kusubiri na kuongeza idadi ya watoto wanaoweza kutibiwa kila mwaka.

Kwa upande wake, Afisa Mgtendaji Mkuu wa Heart Team Africa Foundation, Dkt. Naizihijwa Majani, alisema ufadhili wa NMB umewanufaisha watoto kutoka mikoa 20.

“Kati ya upasuaji 185 uliofanyika mwaka huu, 125 wamefadhiliwa na NMB — jambo linalothibitisha ukubwa wa uhitaji na thamani ya msaada unaotolewa kwa wakati,” alibainisha.

Kwa akina mama Veronica Temba na Asimina Issa kutoka Kilimanjaro, msaada huo umekuwa mwanga wa matumaini. Wakiwa hawana uwezo wa kugharamia upasuaji wa moyo, waliuelezea mchango wa NMB kama “baraka ya kweli” kwa familia zao.

Wameiomba benki hiyo kuendeleza moyo huo wa ukarimu ili familia nyingine nyingi zisizo na uwezo ziendelee kunufaika na ufadhili wa matibabu ya moyo - ufadhili ambao kwa wengi wao ndio tofauti kati ya kukata tamaa na kupata matumaini mapya ya maisha.

Ziara hiyo ilibainisha ukweli muhimu: mpango wa NMB wa kusaidia matibabu ya moyo ya watoto sio tu jukumu la kijamii — ni uwekezaji katika kizazi kijacho cha Tanzania, na katika maisha ya watoto ambao vinginevyo wangeachwa bila matumaini.


No comments:

Post a Comment