
Papa Leo, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, siku ya Alhamisi Desemba 18, 2025 amewakemea vikali viongozi wa kisiasa na viongozi wa dini wanaotumia imani za kidini kuhalalisha migogoro, vita au sera za utaifa, akisema kitendo hicho ni kufuru na dhambi kubwa inayomkosea heshima Mungu.
Katika ujumbe wake uliotolewa kuelekea Siku ya Amani Duniani ya Kanisa Katoliki, itakayoadhimishwa Januari Mosi, 2026, Papa Leo ambaye ni Papa wa kwanza kutoka Marekani hakumtaja kiongozi yeyote moja kwa moja, lakini alitoa wito kwa waumini wote kupinga matumizi mabaya ya dini katika siasa.
“Kwa bahati mbaya, imekuwa kawaida kuona lugha ya imani ikiburuzwa katika mapambano ya kisiasa, kubariki utaifa na kuhalalisha vurugu na mapambano ya silaha kwa jina la dini,” amesema Papa Leo.
Papa Leo amesema, wapo baadhi ya viongozi wa dini ambayo wamekuwa wakitumia dini kama daraja la kuchochea chuki kwa waumini, huku wao wakitafsiri matukio hayo kama uzalendo, jambo ambalo amelikemea. Kutokana na hali hiyo, Amesisitiza kuwa waumini wanapaswa kupinga mwenendo huo kwa vitendo na kwa maisha yao ya kila siku.
“Waumini lazima wapinge kikamilifu, hasa kwa ushuhuda wa maisha yao, aina hizi za kufuru zinazolivunjia heshima jina takatifu la Mungu,” ameongeza.
Katika ujumbe huo wa kurasa nne unaotolewa kila mwaka, Papa Leo pia amelalamikia ongezeko la matumizi ya kijeshi duniani, akinukuu takwimu za Taasisi ya Stockholm ya Utafiti wa Amani (SIPRI) zinazoonesha kuwa matumizi ya kijeshi duniani yaliongezeka kwa asilimia 9.4 mwaka 2024, na kufikia jumla ya Dola za Marekani trilioni 2.7, sawa na asilimia 2.5 ya Pato la Taifa la Dunia (GDP).
Papa Leo, aliyechaguliwa mwezi Mei kuchukua nafasi ya Papa Francis aliyefariki, ameendelea kusisitiza mara kwa mara hatari za kutumia dini kama chombo cha kuhalalisha vurugu.
Katika safari yake ya kwanza nje ya nchi kama Papa, aliyoifanya nchini Uturuki mwezi uliopita, aliwaambia viongozi wa Kikristo Mashariki ya Kati kuwa lazima “wakatae kwa nguvu matumizi ya dini kuhalalisha vita, vurugu au aina yoyote ya misimamo mikali.”

No comments:
Post a Comment