
Na James K. Mwanamyoto
Waziri wa Nchi, Ofisi wa Waziri Mkuu - TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewaelekeza Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari na Msingi nchini kuhakikisha wanadhibiti changamoto ya utoro kwa wanafunzi na walimu katika shule wanazozisimamia.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo, wakati akifungua Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), uliofanyika Jijini Arusha katika Ukumbi wa Tanzania Convention Center (Ngurudoto Mountain Lodge).
“Walimu Wakuu nendeni mkadhibiti utoro wa wanafunzi na walimu shuleni, wapo baadhi ya walimu wakiripoti kazini asubuhi baada ya muda mfupi wanaenda kufanya kazi ya bodaboda mtaani,” Prof. Shemdoe amesisitiza.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, Walimu Wakuu wakidhibiti utoro shuleni watakuwa wamelihakikishia taifa kupata wanafunzi wenye ufaulu mzuri, nidhamu bora, ujuzi wa maisha na moyo wa kizalendo.
Ameongeza kuwa, utoro unasababisha anguko la kitaaluma katika taifa, hivyo Walimu Wakuu wanapaswa kudhibiti utoro wa wanafunzi na walimu ili kutengeneza rafiki ya kuinua kiwango cha taaluma nchini, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha vijana kufikia ndoto zao.
Akizungumzia suala la walimu kuwa na vyanzo mbadala vya kuongeza kipato, Prof. Shemdoe amesema kwamba Serikali haikatazi watumishi kuwa na shughuli mbadala za kuwaongezea kipato, iwapo shughuli hizo zitafanywa na watumishi mara baada ya muda wa kazi wa Serikali.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Shule kuwa chachu ya kuwapatia watanzania tabasamu la kweli kwa kudhibiti utoro wa wanafunzi na walimu, ambao kitaaluma ni kikwazo cha wanafunzi kupata ufaulu mzuri.
Kwa maelekezo haya, Prof. Riziki Shemdoe ameunga mkono kwa vitendo jitihada za Serikali za kuendelea kuchukua hatua madhubuti ya kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na ubora wa elimu nchini.





No comments:
Post a Comment