
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza mamlaka zinazohusika kuchukua hatua kali dhidi ya muuguzi mmoja mkoani Tabora anayedaiwa kufanya upasuaji wa mgonjwa nyumbani kwake kinyume na maadili ya taaluma ya afya.
Akizungumza Machi 4, 2026 alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Machinga jijini Dodoma baada ya kusimamishwa na wafanyabiashara hao, Waziri Mkuu alisema haiwezekani mtu kufanya upasuaji nyumbani wakati Serikali imejenga hospitali, vituo vya afya na hospitali za rufaa katika maeneo mbalimbali ili wananchi wapate huduma salama.
“Sasa naelekeza mamlaka zinazohusika: huyu si wa kuhamishwa, afukuzwe kazi mara moja. Na akishafukuzwa apelekwe kwenye mkono wa sheria. Na wale wanaotoa vibali vya kitaaluma wamnyang’anye hicho kibali. Kidogo kidogo tutaelewana,” amesema.
Aidha, Dkt. Mwigulu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuhakikisha mtumishi huyo anakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria mara moja.
“Mkuu wa Mkoa wa Tabora mkamateni, msimwachie. Afukuzwe kazi, aondolewe hiyo hadhi ya tabibu aliyopewa na pia afikishwe kwenye mkono wa sheria,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita kufanya uchunguzi kuhusu madai ya ubadhirifu wa fedha katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Nyang’wale.
Amesema amepata taarifa kuwa baadhi ya watu wanatengeneza mianya ya ubadhirifu kwa kuwatafuta mafundi na makandarasi wao ili kugawana fedha za umma.
“Sasa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Geita nenda kachunguze pale Nyang’wale ninahitaji hiyo taarifa ili niweze kuwaamulia wale wanaotanguliza fedha ya umma kwa maslahi yao,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara katika masoko nchini ili kuwasaidia kufanya shughuli zao katika mazingira bora.
Amesema katika bajeti ijayo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongeza asilimia tano kwenye mfuko wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ili kusaidia kuboresha miundombinu ya masoko.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewapa mwezi mmoja wafanyabiashara wa Soko la Machinga jijini Dodoma kuhakikisha wanafanya mkutano mkuu na kukamilisha uchaguzi wa viongozi wapya wa soko hilo ili kuweka uongozi halali.
“Ndani ya mwezi mmoja mkutano ufanyike na ndani ya mwezi huo huo uchaguzi ufanyike. Leo ni tarehe 4, hivyo ifikapo tarehe 4 mwezi wa 4 mkutano na uchaguzi viwe vimekamilika ili soko liwe na uongozi utakaosaidia kuratibu shughuli na kufuatilia hoja za wafanyabiashara kwa utaratibu,” amesema.




No comments:
Post a Comment