Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Haruni Mapesa amewataka Wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa Chuo hicho kuhakikisha wanafuata Kanuni, Taratibu na Sheria za Chuo kama zilivyo na zinavyoelekezwa.
Prof. Mapesa ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 2025/2026 kwenye kikao kilicholenga kuwakaribisha rasmi wanafunzi hao ambapo pamoja na mambo mengine alielezea historia ya Chuo, Mipango na Maendeleo ya Taasisi kwa Ujumla wake.
Mkuu huyo wa Chuo amewataka Wanafunzi kuwa na nidhamu kwa kufuata sharia na kanuni za ufanyaji wa mitihani, nidhamu katika Mavazi, kuheshimiana baina yao, lakini pia kuwa na nidhamu kwa Wafanyakazi wanaohudumu katika Taasisi hiyo.
Pia Prof. Mapesa amewasihi sana Wanafunzi wa Chuo hicho kujiepusha na matendo maovu ikiwemo kujihusisha na makundi yasiyofaa, kujiepusha na utumiaji wa dawa za kulevya, pamoja na kuhakiksiha changamoto walizonazo wanaziwasilisha sehemu husika ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati badala ya kufanya vurugu.
“ Jukumu lililowaleta Chuoni ni kusoma kwa bidii na kuhakikisha mnafaulu vyema mitihani kwani ndiyo kipimo cha uelewa wa kile ambacho mtakuwa mmefundishwa, lengo likiwa ni kufikia malengo na matarajio mliyojiwekea katika kutimiza ndoto zenu mlizojiwekea katika maisha.”alisisitiza Prof. Mapesa.
Prof. Mapesa amewataka Wanafunzi hao kuzingatia na kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho muda wote wanapokuwa Chuoni, kuhakikisha wanakamilisha Usajili, kutunza Mazingira pamoja na Miundombinu mbalimbali iliyopo Chuoni.
Kwa upande wake Rais wa Serikali ya Wanafunzi Magashi Magina amewataka Wanafunzi wenzake kuzingatia yale yote yaliyoelekezwa na Mkuu wa Taasisi, ili kujiepusha na usumbufu usio wa lazima.
Kupitia kikao hicho, Wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali ambayo yalipatiwa majibu na viongozi kupitia kikao hicho,Kikao hicho kimehudhuriwa na Menejimenti ya Chuo, Serikali ya Wanafunzi, Wafanyakazi Waendeshaji na Wanataaluma.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano na Masoko
CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE
11.12.2025




No comments:
Post a Comment