WAZIRI MKUU AKAGUA UKARABATI WA SOKO LA MAJENGO NA KUELEKEZA UKAMILIKE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, December 11, 2025

WAZIRI MKUU AKAGUA UKARABATI WA SOKO LA MAJENGO NA KUELEKEZA UKAMILIKE



Na James K. Mwanamyoto - Dodoma


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ametembelea Soko la Majengo jijini Dodoma na kukagua maendeleo ya ukarabati wa soko hilo, ambapo amemuelekeza mkandarasi Kampuni ya Azhar Construction kukamilisha ukarabati huo ifikapo Mwezi Februari 2026 ili wafanyabiashara waanze kulitumia.

Katika kuhakikisha maelekezo yake yanatekelezwa, Dkt. Mwigulu amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Dkt. Frederick Sagamiko kufanya makubaliano ya kimaandishi na mkandarasi huyo kuwa, hakutakuwa na nyongeza ya muda wa ukarabati wa soko hilo ifikapo Mwezi Februari, 2026.

“Serikali inataka ukarabati wa Soko ukamilike kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa Jiji la Dodoma, ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya kuendelea kukuza uchumi wa wafanyabiashara,” Dkt. Nchemba amesisitiza.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa ukarabati wa soko hilo la Majengo unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC).

Akieleza historia ya soko hilo la Majengo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa, soko hilo linalokarabatiwa ni la muda mrefu lilojengwa kipindi cha uhuru (1960’s) hivyo lilikuwa chakavu kiasi cha kutokidhi mahitaji ya sasa kwa muundo wake.

Mhe. Senyamule amefafanua kuwa, ukarabati wa soko hilo ulianza Mwezi Machi 2025 na ukarabati wake unategemewa kukamilika ifikapo Machi 25, 2026, hivyo ofisi yake inaendelea na juhudi za kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati licha ya maendeleo ya utekelezaji wake kutoendana na muda uliopangwa kimkataba.

Naye, mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Majengo, Bw. Abubakari Athuman amemshukuru Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kufanya ukaguzi wa ukarabati katika Soko la Majengo na kumuelekeza mkandarasi akamilishe ukarabati kwa wakati ili waweze kulitumia soko hilo kwani hivi sasa wanafanya biashara katika mazingira ambayo sio rafiki kibiashara.

Kwa upande wake, mfanyabisahara mwingine Bi. Khadija Abdallah amesema kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Mchemba, wafanyabiashara wamepata faraja kuwa mkandarasi atakamilisha ukarabati wa soko ili waanze kulitumia, ikizingatiwa kwamba mvua za masika zitaanza muda si mrefu.





No comments:

Post a Comment