
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Tanzania Premier League Board (TPLB) imeitoza faini ya Shilingi milioni 30 klabu ya Young Africans SC kufuatia makosa mbalimbali yaliyojitokeza katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Simba SC uliochezwa Mei 3, 2026 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TPLB baada ya kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichofanyika Mei 9, 2026, Yanga imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuwasili uwanjani ambapo ilifika saa 10:35 alasiri badala ya saa 10:30 alasiri, jambo lililotajwa kwenda kinyume na Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
Aidha, klabu hiyo imetozwa faini ya Shilingi milioni 30 kutokana na wachezaji na maofisa wake wa ufundi kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia katika uwanja huo na badala yake kutumia nyumba iliyopo nje ya uwanja, kitendo kilichokiuka Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Young Africans SC, Walter Harson amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Shilingi milioni moja kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa Simba SC, Clatous Chama katika mchezo huo.
Pia, shabiki wa Yanga aliyefahamika kwa jina la Mohamed Ally Mposo amefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi 12 baada ya kuingia eneo la kuchezea wakati wa mapumziko na kufanya vitendo vilivyotafsiriwa kuwa ni kinyume cha maadili ya michezo.
TPLB imesema adhabu zote hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni mbalimbali za Ligi Kuu ya NBC zinazohusu taratibu za mchezo, maamuzi pamoja na udhibiti wa klabu na maofisa wa ufundi.




No comments:
Post a Comment