
Na Mwandishi Wetu, Moshi
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Nzowa ameishukuru serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuruhusu michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI).
Bw. Nzowa aliyekuwa mgeni rasmi leo tarehe 12 Desemba, 2025 kwenye mkutano mkuu wa SHIMIWI unaoendelea kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro amesema serikali imetoa fursa ya kushiriki kwenye michezo ikitambua faida zake za kuwa na michezo mahala pa kazi.
“Ninaishukuru sana serikali kwa kuruhusu michezo ya SHIMIWI kufanyika kila wakati, na hata nyie mmekuwa mkifuata taratibu na kalenda yenu mliyoiweka kwa matukio yenu, hongereni sana,” amesema Bw. Nzowa.
Hatahivyo, amewataka washiriki kuhakikisha wanaonesha nidhamu ya juu katika matukio mbalimbali ya shiririkisho hili.
Halikadhali, Bw. Nzowa ametoa angalizo kwa klabu shiriki kuhakikisha wanafanya maandalizi ya kutosha ya kushiriki kwenye michezo hiyo mara wapatapo mwaliko wa kushiriki, ili waweze kufanya vizuri.
“Hili la watumishi kukosa maandalizi mazuri kuna mawili aidha barua ya mwaliko imechelewa kuwafikia au kiongozi mwenye mamlaka kuamua kutowaruhusu kwa madai ya kuwa na kazi nyingi, suala la ushiriki wa michezo lipo kisheria kwa kuwa inawajengea watumishi afya bora na kuwafanya wawe na bidii katika kazi za kuwahudumia wananchi,” amesema Bw. Nzowa.

Awali kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Daniel Mwalusamba amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuruhusu watumishi wa umma kufanya mazoezi na kushiriki michezo mahali pa kazi kwa kujenga afya zao na kuwawezesha kushiriki vyema kwenye kazi za kujenga taifa.
Bw. Mwalusamba, pia amemshukuru mgeni rasmi kwa kuitikia wito wa kushiriki kwenye mkutano huu ambao upo kikatiba, kwani amewapa faraja viongozi wa michezo na pia kuwapa chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii, wanaamini uongozi thabiti wa RAS utaendelea kuwaongoza vyema katika utendaji kazi.
“Nisiwe mchoyo wa fadhila ninawashukuru viongozi wa mahala pa kazi kwa kuendelea kuwaruhusu watumishi wao mahala pa kazi kuja kushiriki matukio mbalimbali ya SHIMIWI, na tunawaomba waendelee kuwa na moyo huo, na pia tunaishukuru ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kufanikisha bega kwa bega mkutano huu, ambao umefanikiwa,” amesema Bw. Mwalusamba.




No comments:
Post a Comment