
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, OWM–TAMISEMI, Mhe. Profesa Riziki Shemdoe, amemuagiza Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI kuwasimamisha kazi Mkuu wa Idara ya Fedha na Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Lugalo.
Shule hiyo, ambayo imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 4.7 na haijakamilika ikiwa ni tofauti na miradi mingine ya aina hiyo ambayo imetekelezwa kwa takribani shilingi bilioni 4.45 na kukamilika kama ilivyopangwa.
Mhe. Kwagilwa ametoa maelekezo hayo baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo na kubaini kasoro zinazoonyesha kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa fedha na utekelezaji wa mradi.
Mhe. Kwagilwa amemuelekeza Katibu Mkuu kuunda timu ya wataalamu kutoka OWM-TAMISEMI kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha taarifa kamili ndani ya wiki mbili.
“Watumishi wa umma, hasa walio chini ya Wizara yetu ya TAMISEMI, jifunzeni kuziheshimu na kuziogopa fedha za umma zinazoletwa kwa ajili ya kufikisha huduma kwa wananchi,” amesema Mhe. Kwagilwa.
Wakati huo huo, Naibu Waziri huyo amemuagiza Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI kuwapangia majukumu mengine Maafisa Elimu Sekondari na Msingi, Maafisa Elimu Taaluma Sekondari na Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Mhe. Kwagilwa yupo mkoani Iringa kukagua miradi ya maendeleo inayosimamiwa na OWM-TAMISEMI ikiwemo miradi ya Elimu.






No comments:
Post a Comment