
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Reuben Kwagilwa, amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kutenga fedha kwa ajili ya kufanikisha mafunzo elekezi kwa viongozi wateule na watumishi kupitia Mfumo wa Mafunzo ya Kielektroniki (E-Learning )unaotumiwa na Chuo cha Serikali za Mitaa.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa viongozi na watumishi katika kutatua changamoto mbalimbali pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Kwagilwa ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Profesa Riziki Shemdoe, wakati wa mahafali ya 17 ya Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, amesisitiza kuwa mfumo huo wa mafunzo ni wa gharama nafuu na unaweza kuwafikia watumishi wengi kwa muda mfupi katika halmashauri zote nchini.
“Naziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini, kukitumia chuo hiki katika kuwajengea uwezo viongozi wa kisiasa, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi wa kada mbalimbali ndani ya utumishi wa umma,” amesema Mhe. Kwagilwa.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kukitumia chuo hicho kama taasisi kiongozi katika kuwajengea uwezo viongozi na watumishi wa umma ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa manufaa ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kwagilwa amewasihi wahitimu kuwa waadilifu, wazalendo na wenye kuzingatia maadili ya kazi wanapoanza safari yao ya kitaaluma na utumishi wa umma.







No comments:
Post a Comment