
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akimkabidhi cheti mwanafunzi aliyefanya vizuri zaidikatika masomo Bw. Mushobos Benjamin Nelson, katika Mahafali ya 39 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Duru ya Pili, yaliyofanyika Kitumba – Kisesa, Katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa, jijini Mwanza. Katikati ni Mkuu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Profesa. Hozen Mayaya.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), (mwenye joho jekundu), akiongoza Maandamano ya Kitaaluma, wakati wa Mahafali ya 39 ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Duru ya Pili, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza, ambapo Mhe. Mhandisi Munde, alikuwa Mgeni Rasmi, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Mussa Khamis Omar (Mb). Kulia ni Mkuu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Profesa. Hozen Mayaya na kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Prof. Joseph Kuzilwa.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akizungumza na wahitimu na washiriki wa Mahafali ya 39 ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Duru ya Pili, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza, (hawapo pichani), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Mussa Khamis Omar (Mb).

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiteta jambo na Mkuu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Profesa. Hozen Mayaya, wakati wa Mahafali ya 39 ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Duru ya Pili, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Prof. Joseph Kuzilwa, akizungumza na wahitimu kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kwa ajili ya kutunuku shahada mbalimbali, katika mahafali ya 39 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Duru ya pili, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza.

Baadhi ya wahitimu wakivaa kofia baada ya kutunukiwa ngazi mbalimbali za cheti katika mahafali ya 39 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Duru ya pili, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza.

Baadhi ya wahitimu wakifurahia baada ya kutunukiwa ngazi mbalimbali za Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili, katika mahafali ya 39 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Duru ya pili, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza.

Meza kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), ikiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa ngazi ya shahada ya uzamili katika mipango ufuatiliaji na tahmnini ya miradi, katika mahafali ya 39 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Duru ya pili, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiwatunuku wahitimu wa ngazi mbalimbali wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) jijini Mwanza, (hawapo pichani), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Mussa Khamis Omar (Mb).

Mkuu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Profesa. Hozen Mayaya, akiteta jambo na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Taaluma Utafiti na Ushauri Elekezi Prof. Provident Dimoso, (kulia), katika mahafali ya 39 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Duru ya pili, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza.
(Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, WF, Mwanza)
Na. Ramadhani Kissimba na Saidina Msangi, WF, Mwanza.
Serikali imewahakikishia vijana wanaohitimu masomo katika vyuo mbalimbali nchini kuwa itaendelea kuimarisha mazingira ya elimu, ajira, teknolojia na ujasiriamali ili kuhakikisha vijana wanatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Hayo yalibainishwa jijini Mwanza, na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), ambaye alimwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 39 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Duru ya Pili, yaliyofanyika Kitumba – Kisesa, Katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa, mkoani Mwanza.
Alisema vijana ni kundi muhimu katika ukuaji wa uchumi na kwa kutambua hili Serikali imeendelea kuwawezesha vijana na wanawake kupitia mikopo, elimu, uwekezaji na miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na mikopo ya asilimia 10 katika Halmashauri.
Aliongeza kuwa Serikali pia imeanzisha madirisha maalumu ya uwekezaji kwa vijana, na kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kufikia shilingi bilioni 916.7 kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Aidha, alisema Serikali imefufua Mfuko wa Utamaduni ambapo zaidi ya miradi 300 ya sanaa ya vijana imenufaika, sambamba na kuwawezesha vijana kushiriki kilimo cha kisasa kupitia programu ya Building Better Tomorrow (BBT) pamoja na fursa zilizopo kupitia sheria ya Ununuzi wa Umma ambapo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza taasisi zote za umma kutenga asilimia 30 ya manunuzi yote kwa ajili ya makundi maalumu wakiwemo vijana.
‘‘Ni muhimu vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma, ambapo asilimia 30 ya manunuzi imeelekezwa kwa makundi maalumu yakiwemo ya vijana, kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza ushiriki wa vijana katika uchumi wa Taifa letu, kukuza ujasiriamali, na kupunguza ukosefu wa ajira nchini. .’’alisisitiza Mhe. Munde.
Mhe. Munde aliwasihi vijana kuendelea kujifunza, kuepuka maambukizi ya UKIMWI, kujiunga na mitandao ya kitaaluma na kuwekeza katika maadili na uzalendo ili kuijenga Tanzania yenye nguvu, yenye maendeleo na inayokimbizana na mabadiliko ya dunia ya sasa.
‘’Mahafali ni ishara kuwa wahitimu wako tayari kuanza safari mpya ya kutumia elimu waliyoipata chuoni, iliyochanganya nadharia na vitendo, kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, hasa katika maeneo ya vijijini ili kuchangia katika kukuza Uchumi wa Taifa’’ Alisema Mhe. Munde.
Pia Mhe. Munde alilipongeza Baraza la Uongozi kwa kufanikisha maendeleo makubwa ya Chuo hicho, na akaahidi kuwa Serikali itaendelea kukiwezesha kibajeti ili kuboresha miundombinu na rasilimali watu.
‘‘Serikali inataka kukifanya Chuo hiki kuwa kitovu cha mawazo ya kimkakati kwa maendeleo ya Taifa hivyo nashauri Chuo kutumia uzoefu wa Kituo cha Mafunzo cha Mwanza kuanzisha vituo vingine katika Kanda ya Pwani na Nyanda za Juu Kusini ili kusogeza huduma za kitaaluma kwa Watanzania wengi zaidi, alisema Mhe. Munde.
Aidha Mhe. Munde alikipongeza Chuo kwa kuanzisha Kituo cha Ubunifu na Ujasiriamali ambacho kimetoa fursa kwa vijana kuanzisha biashara na kubuni suluhisho la changamoto za jamii kwa kuwa ubunifu na ujasiriamali ni injini ya uchumi wa kisasa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Profesa Joseph Kuzilwa, alisema kuwa kupitia Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa, Chuo kimekuwa miongoni mwa Taasisi za Elimu ya Juu hapa nchini ambazo zimegusa maisha ya wananchi wa maeneo ya vijijini kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Aidha, Profesa Kuzilwa aliongeza kuwa mnamo tarehe 29 Agosti, 2025 Chuo kimefanikiwa kuanzisha Kituo cha Ubunifu na Ujasiriamali cha Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (Mipango Entrepreneurship and Innovation Centre) maarufu kama MEI.
‘’Kuanzishwa kwa Kituo cha Ubunifu na Ujasiriamali cha Chuo cha Mipango (Mipango Entrepreneurship and Innovation Centre) na Kituo cha Umahiri (Centre of Excellence) kwa ajili ya wanafunzi vitasaidia sana baadae wanafunzi kutoa mchango stahiki katika maendeleo yao binafsi pamoja na jamii inayozunguka Chuo, jamii zao, na Taifa kwa ujumla’’. Alisema Profesa Kuzilwa.
Naye Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen Mayaya alisema kuwa Chuo kimejipanga katika kuwaandaa wataalamu wenye weledi wa kutosha katika fani za mipango ya maendeleo na kutoa wataalamu wenye uzalendo na waadilifu kwa kuwa uzalendo na uadilifu ndizo nyenzo muhimu katika ujenzi wa uchumi wa nchi.
Alisema katika kufanikisha lengo la Vyuo vya elimu ya Juu na vya kati kuwa vya kimataifa, Chuo kilianzisha dawati la Umataifishaji kwa minajiri ya kuwa na uhusiano na taasisi za nje ya nchi na kupata jukwaa la kubadilishana uzoefu kimataifa.
Profesa Mayaya aliongeza kuwa katika kuimarisha lengo la Umataifishaji Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kimefanikiwa kusaini hati za makubaliano (MoU) mbalimbali ikiwemo hati ya makubaliano na Chuo Kikuu cha Eswatini pamoja na Kituo cha Mananga cha Ujumuishaji wa Kanda na Maendeleo ya Usimamizi (Mananga Centre for Regional Integration and Management Development).
Katika kutekeleza kiu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya Vyuo vya elimu ya Juu na vya kati kuwa vya kimataifa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini kimeona ni vyema kuingia makubaliano na vyuo vingine duniani ambapo itasaidia kukuza masuala ya masuala ya taaluma, utafiti na miradi ya maendeleo. Alisema Profesa Mayaya.
Katika Mahafali ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Duru ya Pili, wahitimu 2,621 kati yao wanaume 1,117 na wanawake 1,504 walitunikiwa Astashahada, Shahada, Shahada ya kwanza na Shahada ya uzamili katika maendeleo ya jamii, Mipango ya maendeleo vijini, Mipango ya maendeleo ya Mikoa, Uchumi, Mipango na usimamizi wa iradi na Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi.

No comments:
Post a Comment