
Na Mwandishi Wetu, Hanang
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa kutokana na hatua ambayo moto umefikia, Serikali imeanza maandalizi ya kutumia teknolojia za kisasa katika kudhibiti moto unaoendelea kuwaka katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia ya Mlima Hanang, mkoani Manyara.
Dkt. Kijaji mesema hayo leo wakati wa ziara yake ya kukagua athari zilizotokana na moto huo, ambao ulianza kuwaka tarehe 3 Desemba 2025 na hadi sasa unaendelea kuelekea maeneo ya juu ya mlima.
Dkt. Kijaji amesema kuwa licha ya jitihada kubwa zilizofanywa katika kudhibiti moto huo, bado kasi yake ni kubwa na hivyo Serikali iko mbioni kupeleka vifaa vya kisasa ili kuuzuia usienee na kuharibu eneo kubwa zaidi la msitu huo wa asili.
Amefafanua kuwa hadi sasa moto huo tayari umetetekeleza ekari 228.5 na ameipongeza Serikali ya Wilaya kwa kazi nzuri waliyofanya katika hatua za awali. Hata hivyo, ameongeza kuwa kutokana na ukubwa wa changamoto, Serikali itachukua hatua za haraka zaidi.
“Moto huu sasa ni janga. Hatutakubali kuuacha uendelee kuharibu uoto wa asili, vyanzo vya maji na mazingira yetu. Tumefika mahali pa kusema imetosha,” alisema Dkt. Kijaji.
Akitaja hatua zinazoanza mara moja, amesema kuwa kuanzia jioni ya leo Serikali itatumia drone ili kupata picha za juu na taarifa sahihi kuhusu mwelekeo wa moto, jambo litakalowawezesha wataalam kupanga mikakati madhubuti ya kuuzunguka na kuudhibiti kabla haujafika kwenye makazi ya watu.
Pia ameelekeza viongozi wa Wilaya kuhakikisha wanawapangia vijana wanaoshiriki uzimaji moto katika vijiji vinavyozunguka mlima, ili waweze kutengeneza mkuza (firebreak) kati ya mlima na makazi ya watu, kuzuia moto kufika kwenye maeneo ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mhe. Almishi Hazali, amesema kuwa hadi sasa vijana 387 wapo eneo la tukio wakishiriki katika shughuli za uzimaji moto, kazi ambayo imeendelea kuimarishwa kadri moto unavyozidi kuenea.
Naye Mbunge wa Hanang, Mhe. Asia Halamga, ameishukuru Serikali kwa hatua za haraka ilizochukua na ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwezesha upatikanaji wa wataalam pamoja na mahitaji muhimu kwa vijana wanaopambana na moto huo.
Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia ya Mlima Hanang, inayosimamiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), ina ukubwa wa hekta 5,836.5.




No comments:
Post a Comment