Na Edward Winchislaus, Dodoma
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) leo disemba 18,2025 kimefanya mahafali yake ya 16 na kuhitimisha jumla ya wanafunzi 9,613 waliotunukiwa shahada mbalimbali za uzamivu, uzamili, shahada za awali na stashahada katik chuo hicho,Kati ya wahitimu hao, wahitimu 9,418 wametunukiwa shahada za awali huku wanafunzi 30 wakipata shahada za uzamivu.
Akizungumza katika mahafali hayo, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Ibrahimu Juma, amewataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kama chachu ya maendeleo kwa kujiandaa kukabiliana na ushindani wa soko la ajira kwa kuzingatia dira za maendeleo ya taifa.
Amesema dira hizo zinaweka mkazo mkubwa katika rasilimali watu wenye ujuzi, hivyo wahitimu wana wajibu wa kuwa wabunifu, kujitambua na kusoma mazingira yanayowazunguka ili kubaini fursa zilizopo badala ya kusubiri kuajiriwa.
“Ni muhimu sana sisi wahitimu tuzisome dira mbili, hii inayomalizika na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili tuweze kufanikiwa katika soko la ajira. Mnapoingia kwenye soko la ajira yasomeni mazingira yanayowazunguka ili mjue fursa zilizopo,” amesema Prof. Juma.
Profesa Juma amesisitiza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaibeba Tanzania ya baadaye mikononi mwa vijana wa sasa, akiwataka wahitimu kuwa tayari kujifunza maisha yote, kutumia teknolojia ya kidijitali na kujenga uwezo wa kufikiri kwa kina ili kuchambua taarifa sahihi na zisizo sahihi, hususan katika enzi ya mitandao ya kijamii.
“Tanzania ya miaka 25 ijayo ni nyinyi, dira zote zinasisitiza rasilimali watu wenye ujuzi, hivyo muwe wabunifu wa kuibua ajira badala ya kusubiri kuajiriwa,” amesisitiza.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Lughano Kusiluka, amesema chuo kinaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa kushirikiana na serikali pamoja na kuendelea na ujenzi wa kituo cha polisi chuoni hapo ili kuimarisha usalama pamoja na hatua za mwisho za kuanzisha kampuni tanzu kwa lengo la kuongeza vyanzo vya mapato ya chuo.
Aliongeza kuwa chuo kinatamani kuona wahitimu wake wakifaulu si tu kitaaluma bali pia katika maisha ya kazi, hivyo amewasisitiza kuwa na nidhamu, juhudi na utayari wa kufanya kazi yoyote halali bila kuchagua, huku akiipongeza serikali kwa kuendelea kuunga mkono ndoto za chuo hicho na wanafunzi wake.
“Tunataka kuona vijana wetu wanafaulu na wanakuwa tayari kufanya kazi yoyote halali bila kuchagua, kwa nidhamu na juhudi,”amesema.
Naye,Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Rwekaza Mkandala, amesema baraza limeendelea kuwa msimamizi mkuu wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya chuo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wadau wa ndani na nje ambapo amesema katika mwaka wa masomo 2024/2025, baraza liliidhinisha sera na miongozo mbalimbali pamoja na kufanya mapitio ya mitaala ili iakisi mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
Hata hivyo, Profesa Mkandala amebainisha kuwa chuo bado kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa rasilimali fedha kutokana na ada kutobadilishwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho, hali inayokifanya chuo hicho kubuni na kuanzisha vyanzo vingine vya mapato.








No comments:
Post a Comment