
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemuelekeza Mkandarasi Jassie and Company (JASCO) anayetekeleza ujenzi wa Daraja la Mkuyuni kukabidhi daraja hilo ifikapo Januari 15, 2026 ili wananchi waondokane na adha wanayopata katika eneo hilo hasa kipindi cha mvua.
Ulega ametoa maelekezo hayo leo tarehe 11 Disemba 2025 Mkoani Mwanza akiwa katika ziara maalum ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo kufuatia agizo la Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba la kumtaka afike eneo hilo na kujua nini changamoto inayosababisha kusuasua kwa ujenzi wa mradi huo.
“Nimetumwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuja hapa Mkuyuni kwa sababu ya ucheleweshwaji wa kazi, nataka niwahakikishie tarehe 15 Januari 2026 nitakuwa hapa na hatutaongeza hata sekunde kwa Mkandarasi hivyo fanya kazi usiku na mchana”, amesema Ulega.
Aidha, Waziri Ulega amegusia kero inayowakumba wananchi wa eneo hilo la uwepo wa vumbi linalosababishwa na shughuli za ujenzi na kumuelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza Eng. Pascal Ambrose kumsimamia Mkandarasi huyo kila siku awe anamwaga maji kuondoa kero ya vumbi kwa wananchi hao.
“Meneja hakikisha hakuna vumbi, maeneo yote haya yamwagwe maji wakati wote, wananchi hawatakiwi kulalamikia vumbi, hilo sio jambo la kujadiliana bali kutekelezwa” ameisisitiza Ulega.
Kadhalika, Ulega amemtaka Mkandarasi huyo kutoa fursa za ajira kwa vijana ili kuwezesha mradi huo kutekelezeka kwa kasi na kumalizika kwa muda uliokusudiwa.
Vilevile, amemtaka kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha amefunga taa za kutosha ili uchumi wa eneo hilo ukue kwa haraka.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Mwanza Mhandisi Pascal Ambrose ameeleza kuwa Mkandarasi huyo anatekeleza mradi huo kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5.1 na mradi ulitarajiwa kukamilika tarehe 13 Novemba 2025 lakini Mkandarasi aliongezewa muda wa siku 76.
Ikumbukwe tarehe 05 Disemba Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alifanya ziara ya kukagua miundombinu mkoani Mwanza na kumuelekeza Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega kwenda mkoani humo kufahamu sababu zinazopelekea mradi wa Daraja la Mkuyuni kusuasua.


No comments:
Post a Comment